DOUGLAS MUTUA: Umaarufu wa Kiswahili na jinsi kinavyofundishwa ughaibuni

DOUGLAS MUTUA: Umaarufu wa Kiswahili na jinsi kinavyofundishwa ughaibuni

Na DOUGLAS MUTUA

NI mwishoni mwa mwaka 2021 tu ambapo Umoja wa Mataifa ulitenga Julai 7 kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, labda kutokana na umaarufu wa lugha hii unavyoenea.

Kwa muda mrefu sana wageni wametokea kuipenda sana, hivyo wamekuwa wakijifunza kwa madhumuni mbalimbali.

Makala hii inahusu ufundishaji wa Kiswahili ughaibuni.

Kiswahili kinavyofundishwa katika vyuo vikuu ni tofauti na kinavyofundishwa kwenye taasisi nyingine za kiufundi na kitaaluma.

Tofauti kuu huwa ni malengo ya kukifundisha.

Kwenye taasisi za kitaaluma, lengo kuu ni kuwawezesha wafanyakazi kutekeleza majukumu yao rasmi.

Hivyo basi, mara nyingi utapata msisitizo wa kufundisha upo kwenye ufasaha wa kuzungumza na kusoma na wala si kuandika.

Mwanafunzi akipita mtihani wa kuzungumza kwa ufasaha na kuelewa kwa kina anaposoma maandishi ndio basi.

Wanafunzi wengi wa aina hii huwa ni wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, maafisa wa ulinzi na usalama, pamoja na wanadiplomasia.

Watalii pia hujitiatia, lakini aghalabu husoma kwa muda mfupi tu kisha wakafunga safari kuelekea Afrika ya Mashariki ili kujipa raha kwa sababu maisha ni mafupi.

Katika vyuo vikuu, kwa sababu ugumu wa kujifunza Kiswahili huchukuliwa kuwa wa wastani, wanafunzi hufurika madarasani kila muhula ili kupata alama nzuri, wengi wakilenga alama ya ‘A’.

Wakishapata alama walizolenga – hakikisho kwamba zikiungwa na za masomo mengine zitawawezesha kutimiza alama nzuri za jumla – wao huondoka ghafla kwenda kufuata masomo mengineyo!

Jambo la kupendeza ni kwamba wapo wanafunzi ambao huingia ndani ya madarasa ya Kiswahili wakinuia kuzoa alama nzuri tu kisha wajiondokee, lakini wakaishia kunata kabisa!

Kisa na maana ni kwamba wanatokea kuipenda lugha yenyewe na utamaduni wa Waswahili, hivyo wakatia nia kuzama kikamilifu kuielewa vyema. Si ajabu kuwaona baadhi yao wakiisoma lugha hii hadi shahada za uzamili na uzamifu.

Utapata vyuo vikuu vingi tu vinavyofundisha Kiswahili kote duniani – kuanzia Asia, Uropa hadi Marekani.

Hata hivyo, Marekani inajulikana kwa kumiliki nyenzo muhimu mno na za kutosha katika tafiti za isimu na fasihi ya Kiswahili.

Kutokana na umuhimu wa Kiswahili kutambuliwa kama lugha inayoweza kutumiwa kuwaunganisha Waafrika wote siku za usoni, mataifa mengi ya Afrika yanakifundisha pia.Kimetokea kuchangamkiwa katika shule na vyuo nchini Rwanda, Burundi, Msumbiji, Afrika Kusini, Botswana, Zambia, Zimbabwe, Ghana na kadhalika.

Nimekutana na wazungu na watu kadha kutoka Afrika Magharibi ambao walijifunza Kiswahili kwa mara ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Ghana.

Chuo hicho kimekuwa na redio inayorusha matangazo kwa Kiswahili.

Kitu kingine cha kupendeza kuhusu ufundishaji wa Kiswahili ughaibuni ni kwamba, japo Kiswahili huzungumzwa na watu wengi zaidi nchini Tanzania ikilinganishwa na Kenya, walimu wengi wanaokifundisha ughaibuni wana asili ya Kenya.

Hali hiyo ni kutokana na mchango wa lugha nyingine katika kufundishia Kiswahili, katika muktadha huu Kiingereza, ambacho ni lugha ya biashara kote duniani. Ushirikiano, na wala si ushindani, katika juhudi za kukieneza zaidi kote duniani utakuwa nguzo muhimu.

Watanzania wamejifunza Kiingereza kuchelewa, na mpaka sasa wanaendelea kujifunza, hivyo wanapata tabu kuwafundisha watu wasioelewana nao kwa vyovyote vile.

Lakini hilo litabadilika kwa sababu Kiswahili kimetuwa tunu ya kutunzwa, hivyo kila mdau anapania kuchangia kukitunzwa kwa kukieneza.

Ushirikiano, na wala si ushindani, katika juhudi za kukieneza zaidi kote duniani utakuwa nguzo muhimu.

mutua_muema@yahoo.com

  • Tags

You can share this post!

Raila kupokea wabunge wa ANC Murang’a

Tundo na Chager nje ya Kajiado Rally, macho kwa Karan Patel

T L