DOUGLAS MUTUA: Vigogo wa kisiasa wasitumie kesi ICC kusababisha mapigano Kenya

DOUGLAS MUTUA: Vigogo wa kisiasa wasitumie kesi ICC kusababisha mapigano Kenya

Na DOUGLAS MUTUA

NI miezi minane pekee kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2022 uandaliwe nchini. Ni wazi kuwa, usipotokea muujiza au maafa, wawaniaji wakuu wa urais watakuwa wawili pekee.

Kando na Naibu Rais Dkt William Ruto na kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Bw Raila Odinga, usitarajie azuke mwaniaji mwingine wa kutetemesha jukwaa la siasa nchini.Wala usidanganyike washirika waliounda muungano wa One Kenya Alliance (OKA) wanaweza kubadilisha mambo kati ya sasa na uchaguzi huo.

Ama wataishia kujiunga na Dkt Ruto katika chama cha United Democratic Alliance (UDA); Bw Odinga au watawania urais iwe yawe tu, wakishindwa washindwe.Kimsingi, wawaniaji wa kuzingatiwa wakati huu ni Dkt Ruto na Bw Odinga. Bila shaka wananchi wenyewe wanajua hili, hivyo ni sharti wawili hao wawe makini sana wakifanya kampeni.

Kenya imewahi kukumbwa na machafuko mabaya ya kisiasa ikabaki na doa hivi kwamba, majirani zetu wa Afrika Mashariki hawaishi kutukumbusha hilo wakinafasika.Hii ina maana kuwa, wanaowania vyeo vikuu wanapaswa kuwa waangalifu sana wanapofanya kampeni ili wasitamke ya kuchochea.

Nimesalitika kuandika haya baada ya kuibuka kwa habari za kuthibitika kuwa huenda Dkt Ruto akashtakiwa upya kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Kisa na maana, mkuu wa mashtaka wa mahakama hiyo amesema amepata ushahidi tosha kuthibitisha Dkt Ruto aliwahonga mashahidi wa upande wa mashtaka na kuporomosha kesi dhidi yake. Kumbuka Dkt Ruto na Rais Uhuru Kenyatta walishtakiwa kwa madai ya kutekeleza dhuluma dhidi ya binadamu kuhusiana na machafuko yaliyozuka nchini baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Wakati wa kampeni zao hizo, walimsawiri Bw Odinga kama adui mkuu aliyetaka wafungwe jela, wakaeneza propaganda mbovu zilizopandisha joto la siasa nchini.Hatimaye kesi dhidi ya Bw Kenyatta iliondolewa kabisa kwa kukosekana ushahidi wa kutosha, nayo ile ya Dkt Ruto ikasitishwa kwa kuwa mashahidi walighairi nia, wakaingia baridi au wakatoweka kimiujiza.

Wakili Paul Gicheru, mwanahabari Walter Barasa na Bw Philip Bett ndio waliodaiwa kuwa mawakala wa Dkt Ruto katika njama ya kuwashawishi mashahidi.Kesi dhidi ya Bw Gicheru inaendelea na ni kutokana nayo ambapo mambo mengi yanadaiwa kufichuka na kuashiria jinsi Dkt Ruto alivyofanikiwa kuvuruga kesi dhidi yake.

Hayo yanayoendelea kwenye ICC, bila shaka, yatakuwa mada kuu katika kampeni kati ya sasa na Agosti mwakani. Lakini sharti wanasiasa wawe waangalifu wasiteketeze nchi.

mutua_muema@yahoo.com

 

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Wakati wa kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko...

Raila alakiwa kishujaa Nyeri akiahidi urafiki wake na jamii...

T L