DOUGLAS MUTUA: Waandamanaji wa Amerika na wa Kenya ni tofauti

DOUGLAS MUTUA: Waandamanaji wa Amerika na wa Kenya ni tofauti

Na DOUGLAS MUTUA

SASA, ukizingatia yaliyojiri Marekani yapata wiki moja unusu iliyopita, umejua kwamba ghasia za baada ya uchaguzi si mtindo wa Kenya au Afrika pekee.

Ghasia zilizuka huko ilipobainika wazi kwa wafuasi wa Rais Donald Trump kwamba hatatumika kwa kipindi cha pili; Bw Joe Biden alishinda uchaguzi uliofanyika Novemba.

Wafuasi wa Trump walikuwa na matumaini kuwa, kutokana na mchakato mrefu wa kuthibitisha matokeo ya uchaguzi, angebatilisha ushinde na kuendelea kutawala.

Matumaini ya aina hiyo nayo yanathibitisha kauli ya wasemao Kimombo kwamba dunia ina wapumbavu wengi na wamesambaa kotekote kwa idadi sawa.

Utawapata popote. Ghasia hizo zilituonyesha kuwa binadamu kokote aliko ana uwezo wa kugeuka nyani wa kuvurumisha mawe na kuharibu mimea ya watu asipodhibitiwa kwa manati na mitego.

Kimsingi, ghasia zenyewe zilitufunza kuwa hisia za binadamu yeyote aliyekerwa na jambo ni za kulipiza kisasi kwa njia za halali na haramu, almradi ijulikane hajaridhika.

Binafsi sikushangazwa na ghasia hizo, kilichonishtua ni ukosefu wa mikakati ya kuzuia uvamizi wa majengo ya serikali, sikwambii kuwabembeleza wavamizi.

Hebu tafakari kuhusu wanaharakati wetu wakivamia bunge kwa maelfu na kukalia kiti cha spika, wavunje ofisi za wabunge na kuiba vitu kwa sababu ya matokeo ya uchaguzi. Najua umejiambia komoyomoyo kwamba hilo haliwezekani Kenya; milio ya bunduki itahanikiza hewani na watu wakatimka mbio, waponywe na miguu yao.

Kwenye tafakuri zako hata umeona damu ya binadamu ikitiririka kama maji kwenye majengo ya bunge! Miili kadhaa pia imelaliana kiholela kwani hilo limegeuka eneo la vita.

Na kwa sababu una ile kasumba ya kikoloni isiyojumuisha Mwafrika ya kudharau chochote cha kiafrika, umejiambia watu wangeuawa hivyo kwa sababu Kenya haithamini raia wake.

Si kweli. Hapo umenoa sana. Walioandamana juzi Marekani waliponea kwa sababu za ubaguzi wa rangi uliokita mizizi kwa miaka mingi.Bahati yao ni kwamba walikuwa wazungu, rangi ambayo polisi wa Marekani hawana mazoea ya kuua kiholela.

Wangekuwa weusi, maandamano hayo yangeingia kwenye kumbukumbu za historia kama umwagaji damu mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo kwa miongo mingi.

Nimeamua kuangazia zaidi hulka ya waandamanaji hao ili nikuthibitishie kwamba binadamu kokote aliko ni mtundu, tofauti ni adhabu inayofuata. Nadhani una habari kwamba walioonekana wakivunja sheria siku hiyo wamekamatwa kwa wingi tu na waliojificha wanaendelea kutafutwa.

Ni msako wa nchi nzima.Sasa zingatia hatua zilizochukuliwa na polisi wa Marekani baada ya maandamano hayo kisha uzilinganishe na za polisi wa Kenya kila kunapotokea maandamano maharibifu.

Kumbuka wauaji na wabakaji waliocheza kwa raha zao wakati wa ghasia za baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 nchini Kenya wangali huru.

Hawatafutwi. Wamesahaulika.Tatizo letu Wakenya liko hapo. Kutoadhibiwa kunatupa hulka ya kutoogopa au kuheshimu sheria. Wamarekani wanajua sheria zao zinavyotekelezwa. Na wanaogopa.

Nikiwa Marekani, kila nikiona madereva wakisubiri kwenye mataa mekundu ili kuwapisha walioonyeshwa mataa ya kijani hukumbuka si kwamba wana adabu, wanaogopa adhabu.

Hitilafu ya umeme inapotokea, hasa kwenye barabara za mitaa, mataa huzimwa na madereva kutarajiwa kutumia akili.Anayetangulia makutanoni huwa wa kwanza kuondoka. Pasipokuwa na polisi, baadhi ya madereva hupita hapo kasi na kusababisha ajali.Kisa na maana? Wanaweza kujitetea kwamba mataa haya

fanyi kazi, hivyo kuna uwezekano wa kuepuka adhabu.Watu wa aina hiyo ukiwahamishia Kenya watakuwa watundu kama sisi tu; hata kupita kasi kwenye mataa mekundu kutageuka mtindo wao kwa sababu hawataadhibiwa.

Kimsingi, ikiwa tunataka kuwa jamii ya wastaarabu, sharti sheria zifanye kazi zilivyo na adhabu zitolewe kikamilifu.

mutua_muema@yahoo.com

You can share this post!

Mshtakiwa ajifungia chooni akiogopa kujua hukumu

Kura za Bobi Wine zaongezeka