Habari Mseto

DP Ruto asisitiza uwaniaji wake wa urais utazingatia amani

May 23rd, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Dkt William Ruto amesisitizia Wakenya kuwa uwaniaji wake wa urais 2022 hautazingatia lolote la ghasia au la taharuki katika sehemu yoyote ya Kenya.

Amesisitiza kuwa hakuna deni lolote analolidai kisiasa kuhusu mwaka 2022 kutoka kwa mrengo wowote kisiasa na badala yake kusisitiza kuwa atawania kama mwaniaji mwingine yeyote na akishindwa aridhike, akiongeza kuwa “ahadi ya Rais Uhuru Kenyatta kwangu kuwa ataniunga mkono ilikuwa tu matamshi ya kisiasa.”

Alisema kuwa katika chama anachowajibikia cha Jubilee kutakuwa na demokrasia huru na ya uwazi kuhusu mwaniaji wa urais, akisema kuwa hategemei kulipwa deni lolote na yeyote katika ulingo wa kisiasa ili atuzwe upeperushaji bendera, bali atategemea ushindani huo ama kupata au kunoa kuwa mwaniaji wa urais.

“Nishindwe, nishinde au iwe namna gani, hakuna mfuasi wangu ambaye nitamkubalia azue fujo kwa niaba yangu,” amesema Ruto.

Huku akilenga mrengo wa Kieleweke ambao unajumuisha wabunge kadha wa Mlima Kenya ambao huungana na wale wa upinzani katika mrengo wa
handisheki kumpinga kisiasa, Dkt Ruto aliwataja kama “wajinga.”

“Hawa wanajifanya kuwa wananielimisha kuhusu jinsi ya kumuunga Uhuru Kenyatta mkono kisiasa ni wajinga… Hao usiwatafute, bali 2022 utawaona wakiingia ndani ya mrengo wa Raila Odinga kisiasa,” amesema.

Alisema kuwa kwa miaka 20 amekuwa akimuunga mkono Uhuru “tukianza ndani ya Kanu kabla ya uchaguzi wa 2002, nikawa ndani ya uwaniaji
wake wa urais 2002, 2013 na mara mbili 2017.”

Alisema kuwa wengi wa walio ndani ya Kieleweke walikuwa hata hawamuungi mkono Uhuru “lakini leo hii ndio hao wanasema kuwa ni walimu wa Ruto kuhusu jinsi ambavyo anafaa kumuunga mkono Rais Kenyatta kisiasa.”

“Wapende wasipende mimi nitabakia mfuasi sugu wa imani ya Kikristo ambayo inanihimiza nijenge kanisa la Mungu kwa rasilimali alizonipa na wale ambao wanateta kuwa nachanga pesa kila wikendi kwa makanisa, waelewe kuwa huwa sichangi pesa zao, wakidhania ni za ufisadi wawasilishe ushahidi kwa wachunguzi na mahakamani,” amesema Ruto.

Kuhusu ukwasi wake ambao huzua maswali ya shaka, alisema kuwa kwa zaidi ya miaka 30 amekuwa mfanyabiashara, mtumishi wa umma na aliyejizolea ‘marafiki wa nguvu’ kote duniani na kwa hivyo “ikiwa wewe hujajipanga kihela, usinichukie nikiwa nimejipanga.”

Dkt Ruto amesema kwa muda mrefu uthabiti wa taifa hili umekuwa ukisambaratika mikononi mwa wale ameita ni matapeli wa kisiasa, madalali na wanaokataa matokeo.

Dkt Ruto alisema kuwa ripoti ya hivi majuzi kutoka tume ya Uwiano wa Kitaifa (NCIC) kuwa huenda kuzuke ghasia katika ngome za Jubilee kuhusu kura mwaka 2022 “ni maoni tu ya wasio na maono mema kwa taifa lao, watu ambao wangetaka kuwe na taharuki ndio waimarike kisiasa.”

Alisema kuwa yeye hababaishwi na siasa zinazomlenga hasa Mlima Kenya kwa msingi wa kumtaja kuwa ni ‘mfisadi’.

“Kuna aliyepoteza pesa zake akazipata katika akaunti yangu? Ufisadi tutapambana nao katika hafla za mazishi au katika mikutano ya hadhara au katika taasisi zinazowajibishwa vita hivyo na katiba ya nchi?” akahoji.

Kuhusu tetesi kwamba kuna mkuu wa kiusalama nchini ambaye anamhujumu kisiasa kupitia kuwaagiza maafisa wa kiusalama nyanjani wasimpe usalama katika hafla zake mashinani, Dkt Ruto alisema hilo halimjalishi kwa kuwa serikali ni kama kampuni kubwa ambayo katika kitengo cha usalama kuna “wazembe, wakora na washenzi.”

Akionekana kumlenga Dkt Karanja Kibicho ambaye hutajwa sana katika agizo hilo la kiusalama dhidi ya Ruto, alisema hilo atalishughulikia kimyakimya ndani ya serikali ikizingatiwa kuwa mimi ni Naibu Rais.