DP yamteua Spika Muturi kuwa mgombeaji urais

DP yamteua Spika Muturi kuwa mgombeaji urais

Na KENYA NEWS AGENCY

CHAMA cha Democratic Party (DP) kimemteua Spika wa Bunge la Kitaifa, Justin Muturi kuwa mgombeaji wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa kitaifa Esai Kioni, wajumbe wa chama hicho Jumatano walisema wamefanya uchunguzi na kubaini kuwa Bw Muturi ndiye anaweza kuongoza eneo la Mlima Kenya na taifa kwa ujumla baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu.

“Tumefanya uchunguzi miongoni mwa wagombeaji urais nchini na kuamua kuwa Justin Bedan Njoka Muturi ndiye atapeperusha bendera yetu ya urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022,” Bw Kioni akasema katika mkahawa mmoja Nyeri.

Wajumbe waliohudhuria mkutano huo walitoka kaunti za Nyeri, Murang’a, Kiambu, Nairobi, Embu, Tharaka Nithi, Meru, Nyandarua na Laikipia.

Bw Kioni alisema Bw Muturi ni kiongozi ambaye ameonyesha tajriba ya uongozi, ni mwadilifu na hivyo anaweza kuongoza taifa hili.

“Spika Muturi ni kiongozi wa umma aliyejitolea na ambaye tunaamini anaweza kuwa mgombeaji wa chama chetu cha DP. Tumemsikia na tunaamini kuwa hatabadili msimamo wake na kwamba atapambana hadi kwenye debe la urais,” mwenyekiti huyo akawaambia wanahabari.

Bw Kioni alimwalika Spika Muturi kujiunga rasmi na chama cha DP, akiongeza kuwa hakuna mgombeaji mwingine wa urais ambaye ni bora kuliko yake.

“Kwa hivyo, leo (Jumatano) tunamwalika Bw Muturi kujiunga nasi ili awe mwanachama rasmi wa DP,” akasema huku akitoa wito kwa wanachama wa chama hicho kuunga mkono Bw Muturi.

You can share this post!

Mabingwa watetezi Man-City wakomoa Wycombe na kutinga hatua...

NGILA: Teknolojia mpya ya mbegu sawa ila wapi hamasisho?