DPP aagizwa kufichua ushahidi wa kesi ya ufisadi dhidi ya Jumwa

DPP aagizwa kufichua ushahidi wa kesi ya ufisadi dhidi ya Jumwa

Na PHILIP MUYANGA

MAHAKAMA imeamuru upande wa mashtaka kufichulia washtakiwa kwa wakati ufaao ushahidi inaonuia kuutumia katika kesi ya ufisadi inayomkabili mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa na watu wengine sita.

Hakimu Mkuu wa Mombasa, Bi Edna Nyaloti pia aliagiza pande zote mbili kuweka sahihi wanapopokezana ushahidi huo ambao utawasilishwa na upande wa mashtaka.

Mahakama hiyo ilitoa maagizo hayo baada ya washtakiwa kupitia mawakili wao kushtumu upande wa mashtaka kwa kuwavamia na ushahidi mpya.

“Kufichua ushahidi kunahakikisha upande wa mashtaka hauwaweki washtakiwa kwa njia ambayo haitakuwa bora kwao,” alisema Bi Nyaloti.

Hakimu huyo aliahirisha kusikizwa kwa kesi hiyo hapo jana baada ya wakili wa upande wa washtakiwa Bw Jared Magolo kuambia mahakama kuwa washtakiwa wawili hawakuwa mahakamani kwa kuwa walikuwa katika sherehe za kidini.

Upande wa mashtaka ulitaka agizo la kukamatwa kwa wawili hao litolewe kwa kukosa kufika mahakamani.Kiongozi wa mashtaka, Bw Alex Akula, alisema kuwa ni mahakama pekee ambayo ina uwezo wa kumruhusu mshtakiwa kutofika mahakamani.

Bi Jumwa anakabiliwa na mashtaka sita ya ufisadi mojawapo likiwa ni njama ya kutaka kuilaghai nchi Sh19 milioni zilizopangiwa hazina ya kitaifa ya maendeleo ya eneo bunge (NG-CDF).

You can share this post!

400 wafa vita kati ya Israeli na Wapalestina vikichacha

Supkem yakana mgawanyiko kuhusu Idd