Habari Mseto

DPP aamriwa awasilishe mashtaka mapya dhidi ya Ongwae

May 24th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Alhamisi alipewa muda wa siku 14 kuwasilisha mashtaka mapya dhidi ya aliyekuwa kinara wa mamlaka ya kukadiria ubora wa bidhaa nchini (Kebs) Charles Ongwae anayekabiliwa na shtaka la kujaribu kuwaua wakulima kwa kuruhusu mbolea iliyo na madini ya Mercury.

Hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot alitoa agizo hilo baada ya kuelezwa na kiongozi wa mashtaka Bw Alexander Muteti kuwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP imekamilisha kuandaa cheti kipya cha mashtaka.

Kiongozi wa mashtaka Alexander Muteti (kati). Picha/ Richard Munguti

Na wakati huo huo washtakiwa watano walisema wako tayari kuendelea na kesi na kueleza mahakama “izingatie kesi hiyo imekaa kortini kwa muda wa mwaka mmoja bila kuanza.”

Washtakiwa hao waliomba mahakama iamuru wapewe ripoti ya mwanzo iliyotolewa na Kebs ikidai mbolea iliyoingizwa nchini na kampuni ya OCP (K) Limited ilikuwa na madini ya Mercury.

Bw Cheruiyot aliamuru afisi ya DPP iwasilishe ushahidi wote uliopokewa na Kebs awali waandae utetezi wao.

Hakimu aliombwa azingatie kuwa kesi imetajwa  mara nyingi na imekumbwa na msururu wa maombi mbali mbali.

Bw Ongwae  ameshtakiwa pamoja na Bw Eric Chesire Kiptoo maafisa wakuu Mabw Peter Kinyanjui, Martin Musyanya na Pole Mwangemi na afisa anayesimamia afya ya umma katika bandari ya Kilindi Erick Kariuki na Benson Oduor ambaye ni ajenti wa kampuni ya upakiaji bidhaa ya Bolloré Transport and Logistics Kenya Ltd.