DPP aamuru polisi kuchunguza video ya uchochezi

DPP aamuru polisi kuchunguza video ya uchochezi

BENSON MATHEKA NA KNA

MKURUGENZi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji, ameagiza polisi kuchunguza kanda ya video inayodaiwa kuvurugwa ili kumsawiri Naibu Rais William Ruto kama aliyechochea chuki za kijamii wiki jana.

Bw Haji alimwandikia barua Inspekta Jenerali wa polisi Hillary Mutyambai akimtaka kufanya uchunguzi kuhusu waliosambaza kanda hiyo kwenye mitandao ya kijamii akisema ina uwezo wa kuchochea chuki za kijamii na kuumiza baadhi ya watu.

“Unaagizwa kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na video hiyo ikiwemo asili, usambazaji na uhalali wake,” Bw Haji alimwagiza Bw Mutyambai.

Alimwagiza kuwasilisha faili ya uchunguzi kwa afisi yake ili ichukue hatua za kisheria iwapo kutakuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya wahusika.

Muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Dkt Ruto ulikuwa umeandikia Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano (NCIC) ukilaumu Gavana wa Mombasa Hassan Joho na Mbunge wa Suna Junet Mohamed kwa kusambaza kanda hiyo.

Wakati huo huo, wabunge watatu kutoka Siaya wameomba asasi za usalama kumhoji Dkt Ruto kuhusiana na karatasi zenye ujumbe wa uchochezi wa kutisha baadhi ya jamii katika kaunti ya Uasin Gishu.

Seneta James Orengo, mbunge wa Ugunja, Opiyo Wandayi na mwenzake wa Gem Elisha Odhiambo walisema naibu rais na washirika wake wanafaa kuhojiwa kufuatia kauli walizotoa majuzi zinazoweza kuzua hofu na uhasama miongoni mwa jamii katika kaunti hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Wazee wakemea wanasiasa kwa kuvuruga Mumias

Mwanamke alilia korti imsaidie kupata Sh29m kutoka kwa sacco

T L