Habari Mseto

DPP aapa kukabiliana na visa vya kutoweka kwa raia

December 10th, 2018 1 min read

Na CHARLES WANYORO

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Nordin Haji ameelezea masikitiko yake kuhusiana na ongezeko la visa vya watu kutoweka na hata kuuawa katika hali ya kutatanisha.

Bw Haji alisema kuwa visa hivyo huenda vikasababisha Wakenya kukosa imani na serikali na hata kuchangia katika ongezeko la magenge ya wahalifu.

Alisema kuwa afisi yake leo inatarajiwa kukutana na mashirika ya kijamiii pamoja na maafisa wa usalama katika juhudi za kutaka kuhakikisha kuwa visa hivyo vinakomeshwa.

DPP alikuwa akizungumza wakati wa maankuli ya kuadhimisha miaka 25 kwa shirika lisilo la kiserikali ambalo huchunguza dhuluma na kutoweka kwa watu la Medico-Legal Unit (IMLU).

Bw Haji alisema kuwa afisi yake itakuwa katika mstari wa mbele kuhamasisha washikadau mbalimbali katika kuhakikisha kuwa visa vya kutoweka na kuuawa kwa watu kiholela katika baadhi ya maeneo humu nchini.

Alisema Kenya imetia saini Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu ulindaji wa haki za kibinadamu.

DPP alisema mkataba huo umepiga marufuku dhuluma dhidi ya binadamu na mauaji ya kiholela.

“Kenya ni nchi ambayo inazingatia utawala wa sheria kwa hivyo suala la kutoweka kwa watu kiholela halifai kuchukuliwa kimzaha,” akasema.

Mkurugenzi wa IMLU Peter Kiama alisema shirika lake limesaidia zaidi ya waathiriwa 5,000 wa ukatili ambao mara nyingi hutekelezwa na maafisa wa usalama.