Habari Mseto

DPP akubaliwa kuwasilisha ushahidi mpya dhidi ya familia ya Ngirita

November 16th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA  imemkubalia Mkurugenzi wa Umma (DPP) Noordin Haji kuwasilisha ushahidi mpya jinsi kampuni za familia ya Ngirita ilivyopokea mamilioni ya pesa katika kashfa ya Sh8bilioni ya shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS).

Hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti alisema “kumnyima DPP fursa ya kuwasilisha ushahidi huo ni kuilemaza kabisa kesi hiyo ya ufisadi.”

Bw Ogoti alimwamuru DPP awakabidhi washukiwa 37 walioshtakiwa nakala za ushahidi huo mara moja.

Hakimu aliwapa washtakiwa muda wa siku nne kusoma ushahidi huo kabla ya kesi kuanza kusikizwa tena Novemba 21, 2018.

Akikubalia ombi la DPP lililowasilishwa na wakili Caroline Kimiri , Bw Ogoti alisema , “Kifungu nambari 50 (2) (J) cha Katiba kinamtaka DPP awape washukiwa ushahidi wote atakaotegemea kuthibitisha kesi dhidi yao.”

Alisema kukubalia ombi la washukiwa hao 37 ya kumzuia DPP kuwasilisha ushahidi huo mpya ni kukubali kuvunja katiba na sheria ambazo mahakama inatakiwa kutekeleza na kuhakikisha imetekelezwa.

Alisema kesi hii dhidi ya aliyekuwa katibu mkuu Bi Lillian Mbogo Omollo , aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NYS Richard Ndubai na washukiwa wengine 37 sio ya kawaida.

Alisema mashtaka ni 82 , washukiwa ni 37 na mawakili ni zaidi ya 30.

Bw Ogoti alisema kifungu nambari 25 cha katiba kimeagiza kila mshukiwa apewe fursa ya kujitetea na kutendewa haki.

Hakimu aliwakubalia viongozi wa mashtaka Bw Gitonga Riungu , Evah Kanyuira, Caroline Kimiri , Jalson Makori na Hellen Mutellah kuwasilisha ushahidi huo mpya.

Ushahidi huo unajumuisha nakala za malipo kwa Bi Phyillis Njeri Ngirita na kampuni ya Njewanga

Pia washtakiwa watapewa nakala za taarifa za Benki ya Kenya Commercial (KCB) tawi la Naivasha.

Na wakati huo huo , hakimu alifahamishwa Bi Anne Wambere Ngirita anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Mater.

Pia alipokea ripoti ya uchunguzi aliofanya Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai kuhusu hospitali Anne alidai alihudhuria Naivasha.

Bw Riungu alisema ripoti za madaktari waliomtibu Anne Wambere Ngirita zilisema anaweza kuendelea na kesi huku akitumia madawa.

Wakipinga kuwasilishwa kwa ushahidi huo, washukiwa hao walimweleza hakimu mkuu Bw Douglas Ogoti , kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) alikiuka kifungu nambari 50 cha katiba kinachomtaka afichue ushahidi wote kabla ya kesi kuanza kusikizwa.

“Ni jukumu la DPP kutimiza vipengee vyote vya Kifungu nambari 50 (2) (c) na (J) cha katiba kinachomtaka amkabidhi kila mshukiwa ushahidi kabla ya kuanza kusikizwa kwa kesi,” Bw Ogoti alifahamishwa.

Mawakili Assa Nyakundi, Migos Ogamba na  Stephen Ligunya walisema hatua ya DPP kuwasilisha ombi la kuwasilisha kwa ushahidi baada ya kesi kuanza kusikizwa ni ukandamizaji wa haki za washtakiwa.

Washukiwa hao wamekanusha mashtaka 82 dhidi yao. Wako nje kwa dhamana.