Habari Mseto

DPP amtaka Boinnet ampe ripoti ya uchunguzi wa mkasa wa Solai kwa siku 14

May 11th, 2018 1 min read

Na ERIC MATARA

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Ijumaa alitaka uchunguzi ufanywe kubaini kiini cha mkasa wa bwawa la Patel eneo la Solai, Nakuru uliotokea Jumatano usiku.

Bw Noordin Haji alimwagiza Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet kuanzisha mchakato huo kutambua iwapo kuna watu walisababisha mkasa huo ulizua vifo vya watu 44 huku ukiharibu makazi na mazingira eneo hilo.Alimtaka Boinnet kuwasilisha ripoti kwa afisi yake katika muda wa siku 14.

“Naagiza uchunguzi uanzishwe na faili ya matokeo yake iwasilishwe kwangu siku 14 zijazo, ili tuchukue hatua zinazofaa,” ikasema taarifa iliyotiwa saini na Bw Haji.Hili linajiri wakati Wakenya wanauliza maswali kuhusu uhalali wa ujenzi wa bwawa hilo kubwa linalomilikiwa na mkulima maarufu Patel Mansukul.

Iliibuka Alhamisi kuwa mabwawa yote kati eneo hilo hayana leseni ya ujenzi.

Mamlaka ya Usimamizi wa Maji (Warma) imesema imekuwa ikijaribu kuifikia kampuni ya Patel Coffee Estates Limited ili kuhalalisha bwawa hilo, lakini juhudi zao zimegonga mwamba.Hii ni baada ya kung’amua hatari iliyokuwa ikiwakodolea macho wakazi walioishi upende wa chini wa bwawa hilo, walipoona maji yakipenyeza.

Meneja wa shirika hilo eneo la Rift Valley, Simon Wang’ombe, alisema maafisa wa Warma wamekuwa wakizuru eneo hilo mara kwa mara.

Alifafanua kuwa sheria inasema kuwa bwawa la kibinafsi lenye urefu wa mita tano juu linahitajika kuhidhinishwa na shirika hilo.

“Kwa mwaka mmoja uliopita, tumekuwa tukijaribu kuwasiliana na maafisa wa kampuni hiyo bila mafanikio. Kulingana nasi, bwawa hili lilijengwa kinyume na sheria,” akasema.

Lakini swali kuu ni, mbona shirika hilo la udhibiti wa mabwawa lilichelewa sana kuokoa hali kabla ya janga hilo kutokea.