Habari za Kitaifa

DPP aomba Kang’ethe azuiliwe gerezani kumzuia kutoroka

February 14th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameiomba mahakama ya Milimani kutoa agizo  la kuzuiliwa kwa mshukiwa Kevin Kang’ethe katika gereza la Industrial Area baada ya kunyakwa tena alipotoroka katika seli za kituo cha polisi cha Muthaiga, Nairobi.

Mshukiwa amefikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Lucas Onyina mnamo Jumatano.

Bw Kang’ethe anayetakiwa nchini Marekani kushtakiwa kufuatia mauaji ya aliyekuwa mpenzi wake, Margaret Mbitu, mnamo Oktoba 31, 2023, alikuwa akizuiliwa Muthaiga kwa muda ambao ungedumu siku 30 tangu Januari 31, 2024, DPP akiendelea na mchakato wa namna ya kumwasilisha nchini Marekani kukabiliwa na mashtaka.

Mkuu wa mashtaka Vincent Monda alimrai Bw Onyina kukubali ombi la DPP kwa sababu mienendo ya Bw Kang’ethe ya kutoroka kituoni Muthaiga bila polisi kutambua ni ishara wazi kwamba hawezi kuaminika.

Bw Monda amesema gereza ndipo pahala salama pa kumzuilia mshukiwa, mchakato wa kumwasilisha nchini Marekani ukiendelea.

Agizo la kukamatwa kwa mshukiwa huyo lilitolewa Ijumaa wiki jana.

DPP pia ameiomba mahakama kuruhusu Bw Kang’ethe kutembelewa na jamaa, mawakili na hata daktari wa serikali endapo watu hao watahitajika kwa sababu ana haki zake za kimsingi ikiwemo haki ya kikatiba na ya kupata huduma za afya.

Bw Monda hata hivyo alisema mshukiwa akitembelewa, basi afisa wa uchunguzi Patrick Wachira awepo.

Lakini mawakili wa Bw Kang’ethe wakiongozwa na Antony Kago na David Muthama wamepinga vikali ombi la DPP wakisema linakiuka agizo la awali kwamba azuiliwe katika kituo cha polisi cha Muthaiga.