DPP apewa siku tatu kuwasilisha ushahidi katika kesi dhidi ya maafisa watatu wakuu wa polisi

DPP apewa siku tatu kuwasilisha ushahidi katika kesi dhidi ya maafisa watatu wakuu wa polisi

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji  amepewa siku tatu kuwasilisha  ushahidi katika kesi dhidi ya maafisa watatu wakuu wa polisi walioshtakiwa na Mbunge wa Gatundu kusini Moses Kuria.

Hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Kennedy Cheruiyot alimtaka Bw Haji awasilishe ushahidi kuwatetea maafisa hao wanaoshtakiwa kwa kukaidi agizo la mahakama.

Bw Kuria anaomba mahakama iwafunge Bi Fatuma Hadi- DCIO Kilimani, aliyekuwa OCPD Kilimani Bw Aden Mohammed na Naibu afisa msimamizi wa kituo cha polisi cha Kilimani (OCS) Martin Fwamba kwa kukaidi agizo wamwachilie huru.

Bw Kuria alikuwa anazuiliwa katika kituo hicho cha Kilimani kwa makosa ya kumpiga na kumjeruhi mwanamke mnamo Januari 10, 2020.Wakili George Omenke anayemwakilisha Bw Kuria aliwasilisha kesi akiomba Bw Kuria aachiliwe.

Bw Cheruiyot aliamuru maafisa wakuu katika kituo cha polisi cha Kilimani kimwachilie huru mwanasiasa huyo.Lakini agizo hilo halikutekelezwa na maafisa hao wa polisi na badala yake wakaendelea kumzuilia mwanasiasa huyo.

Bw Cheruiyot alimwachilia Bw Kuria kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh50,000 na kumwagiza afike kortini Januari 13,2020 kujibu shtaka.Katika ushahidi aliowasilisha mahakamani Bw. Kuria amesema polisi walipokabidhiwa agizo la kumwachilia Bw Aden anadaiwa alikataa kutii maagizo ya mahakama.

Washtakiwa hao, walilamika mbele ya Bw Cheruiyot kuwa DPP hajawakabidhi nakala za ushahidi wao ndipo waandae ushahidi.Wakili wa serikali Martin Munene anayewakilisha maafisa hao watatu wa polisi aliomba mahakama imruhusu DPP awasilishe ushahidi wa kutoa mwanga katika kesi hiyo.

Bw Munene alieleza mahakama Bi Hadi yuko ng’ambo anakopanda mafunzo zaidi katika utenda kazi wa kikosi cha polisi.Bw Cheruiyot aliyesema ni zaidi ya miezi saba tangu amwamuru DPP awasilishe ushahidi katika kesi hiyo atampa fursa ya mwisho kuuwasilisha kabla ya adhabu kupitishwa.

Bw Cheruiyot aliamuru kesi hiyo isikizwe Septemba 15, 2021.

  • Tags

You can share this post!

AFYA: Umuhimu wa mtu kula chakula kwa uwiano unaotakiwa

Mtindo bora wa maisha