Habari za Kitaifa

DPP aomba mahakama imnyime dhamana mwanafunzi aliyeshtakiwa kumjeruhi polisi

June 5th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameomba mahakama imnyime dhamana mwanafunzi wa chuo kikuu anayeshtakiwa kumshambulia polisi akidai usalama wake uko hatarini.

Hakimu mwandamizi Ben Mark Ekhubi alielezwa wananchi walioshuhudia Ian Ngige Njoroge akimzaba makonde na mateke Koplo Jacob Ogendo huenda wakamshambulia mshtakiwa.

Viongozi wa mashtaka Victor Owiti, James Gachoka, Virginia Kariuki na Danstan Omari walisema habari zinazosambaa katika mitandao zinaonyesha umma umeghadhabishwa na kitendo hicho na usalama wa Ngige uko hatarini.

Bw Owiti alisema mtu ambaye yuko na ukakamavu wa kushambulia polisi ni mtu hatari kwa usalama wa kila mmoja katika jamii.

“Anafaa kuzuiliwa hadi kesi isikilizwe na kuamuliwa,” akasema Bw Owiti.

Bw Owiti aliendelea kupinga ombi la dhamana ya mshtakiwa akisema kwamba kesi inayomkabili mshtakiwa ya wizi wa mabavu, kumpiga na kumjeruhi afisa wa usalama na kutoheshimu maafisa wa usalama wa nchi ni nzito.

Ngige alikanusha Jumanne kwamba alimpiga na kumjeruhi Koplo Ogendo na kumnyang’anya simu ya kiunga mbali na kukataa kukamatwa.

Hakimu alifahamishwa mnamo Juni 2, 2024, mshtakiwa alitoroka baada ya kutekeleza uhalifu huo.

“Mshtakiwa alikuwa amejificha kwa muda wa saa nyingi. Alikamatwa ilipoguduliwa alikuwa amejificha kwa mama yake,” Bw Owiti alisema

Mahakama ilielezwa Koplo Ogendo aliomba akubaliwe kutoa ushahidi kabla ya mshtakiwa kuachiliwa kwa dhamana.

Afisa anayechunguza kesi hiyo Josphat Rotich, aliomba muda mshtakiwa azuiliwe ili asiwavuruge mashahidi.

Mahakama ilielezwa kwamba aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko amependekeza kesi hiyo isuluhishwe nje ya mahakama.

“Sonko amechapisha katika mtandao wa kijamii kwamba kesi hiyo inafaa kusuluhishwa nje ya mahakama na Ngige aruhusiwe kuendelea na masomo,” Bw Ekhubi alifahamishwa huku korti ikielezwa kesi hiyo imeingiliwa katika mitandao ya kijamii.

Bw Omari alisema kikosi cha polisi kimefedheheshwa na kisa hiki ikitiliwa maanani polisi wa nchi hii “wamepelekwa kulinda na kutunza amani nchini Haiti na Umoja wa Mataifa (UN)”.

Mshtakiwa alirudishwa rumande hadi Alhamisi wakati mahakama itakapoamua ikiwa itamwachilia kwa dhamana au la.

Ngige ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiufundi (TUK). Alikanusha mashtaka matatu yanayomkabili.