Habari Mseto

DPP apinga mfungwa wa ugaidi kukaa jela siku nane tu!

April 26th, 2024 1 min read

NA RICHARD MUNGUTI

IDARA ya Magereza imeagizwa na Mahakama Kuu isimwachilie gaidi aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka 12 kwa kuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la ISIS.

Jaji Lilian Mutende aliamuru Dkt Mohamed Abdi Ali asalie gerezani hadi kesi iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga akipinga hukumu hiyo ya miaka 12 isikilizwe na kuamuliwa.

Jaji Mutende aliamuru idara ya magereza isithubutu kumwachilia Dkt Ali aliyekamatwa Aprili 29, 2016, kutoka Hospitali ya Makueni.

Akimhukumu Dkt Ali aliyekuwa amepanga kutumia virusi vya kimeta kushambulia nchi hii kigaidi, hakimu mkuu Martha Mutuku aliamuru kifungo cha gaidi huyo kianze kutumika kuanzia Aprili 29, 2016, alipokamatwa.

Kesi hiyo ilichukua miaka minane kukamilika.

Kwa mujibu wa Bi Mutuku, miaka minane ikiondolewa kwa miaka 12, gaidi huyo alikuwa atumikie kifungo cha miaka minne.

DPP kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Duncan Ondimu alisema idara ya magereza ikimpunguzia kifungo, Dkt Ali angetumikia kifungo cha siku nane tu.

“Ikiwa hii mahakama haitaingilia kati, mfungwa huyu ataondoka gerezani Aprili 29, 2024, baada ya kifungo cha miaka 12 kupunguzwa. Atakuwa ametumikia kifungo cha siku nane tu gerezani,” Bw Ondimu alimweleza Jaji Mutende.

Jaji huyo alielezwa kwamba DPP amekata rufaa kupinga hukumu hiyo pamoja na kuomba mahakama imwadhibu gaidi huyo katika mashtaka matatu aliyoachiliwa.

Dkt Ali almaarufu Abu Fidaa almaarufu Abu Shuhadaa almaarufu Abu Ramzi, alipatikana na hatia ya kutoa mafunzo yenye itikadi kali sawia na kuwa mwanachama wa ISIS.