Habari Mseto

DPP aruhusiwa kuwasilisha ushahidi dhidi ya Kidero

July 15th, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Jumatatu aliruhusiwa na mahakama ya kuamua kesi za ufisadi awasilishe ushahidi jinsi Benki ya Cooperative ilivyoagizwa na kaunti ya Nairobi ilipe zaidi ya Sh200milioni wakati Dkt Evans Kidero alikuwa Gavana.

Malipo hayo kwa kampuni kadhaa ikiwamo Ngurumani Traders yalitolewa kati ya 2014 na 2015.

Akimruhusu kiongozi wa mashtaka Riungu Gitonga kuwasilisha ushahidi, hakimu mkuu Douglas Ogoti alisema kifungu nambari 33 cha sheria za ushahidi kinamruhusu DPP kuwasilisha ushahidi wa ziada.

“Namruhusu kiongozi wa mashtaka kuwasilisha ushahidi huo na kuwapa washtakiwa kukiwa na wakati ndipo waandae utetezi wao,” Bw Ogoti alisema hayo.

Mawakili wanaomwakilisha Dkt Kidero, Nelson Havi na Philip Nyachoti walipinga vikali hatua ya afisa anayechunguza kesi hiyo Mulki Umar kumruhusu Bi Lillian Mbeke Kioko , meneja wa Benki ya Cooperative kuwasilisha ushahidi badala ya Bi Charity Karimi William aliyestaafu.

“Tunathibitishia mahakama kwamba Bi Charity Karimi William alistaafishwa na Benki ya Cooperative 2018 na mahala pake pakachukuliwa na Bi Lillian Mbeke Kioko,” Bw Ogoti alifafahamishwa.

Afisa anayechunguza kesi hiyo Mulki Umar aliomba aruhusiwe na mahakama amwasilishe Bi Kioko kutoa ushahidi huo badala ya Karimi.

Umar aliomba korti akubaliwe amtegemee Bi Kioko badala ya Karimi kuwasilisha ushahidi huo.

Hatua hiyo ilipingwa vikali na mawakili wanaomwakilisha Dkt Kidero pamoja na washtakiwa wengine 15 Mabw Nelson Havi, John Mburu na Philip Nyachoti.

Wakili wa Serikali Riungu Gitonga (kushoto). Picha/ Richard Munguti

“Hatukuwa tumearifiwa jambo hili. Shahidi ambaye hakuwa ameandikisha taarifa hawezi kukubaliwa kutoa ushahidi katika kesi hii,” alisema Havi.

Hakimu alielezwa maagizo aliyotoa kabla ya kesi ya Dkt Kidero kuanza kusikizwa yalikuwa ushahidi wote ukabidhiwe washukiwa wajiandae.

Hakimu alisema kuwa maagizo aliyotoa yamo wazi na kwamba “ lazima DPP afanye maombi mapya kabla ya kuwasilisha ushahidi mpya.”

Baada ya kumruhusu Bw Gitonga kuwasilisha ushahidi huo, meneja wa Benki kuu ya Kenya Leonard Kimutai Kipsanai aliwasilisha ushahidi kutoka Benki kuu ya Kenya (CBK) jinsi kaunti ya Nairobi ilivyolipa kampuni ya Ngurumani zaidi ya Sh3milioni.

Bw Kipsanai aliwasilisha ushahidi na kusema CBK “ iko na rekodi za malipo ya kaunti zote 47 kupitia kwa mtandao wao wa Kenya Electronic Payment and Settlement System (Kepss).”

“CBK imeweka rekodi ya kaunti zote za malipo ya fedha zote kutoka kwa kila benki,” alisema Bw Kipsanai.

Alisema taarifa hiyo ya malipo ya Ngurumani yalitayarishwa na meneja mwingine Bi Sophy Langat.

Dkt Kidero amekanusha mashtaka ya kulipa kwa njia ya ufisadi makampuni yaliyodaiwa yalitoa huduma kwa kaunti hiyo.

Kesi inaendelea.