Habari Mseto

DPP ataka kesi ya Wachina 2 kuhusu ulanguzi wa watoto ifutwe

October 18th, 2018 1 min read

Na Brian Ocharo

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji ametaka kesi ambapo raia wa Uchina na Wakenya wawili wameshtakiwa kuhusu usafirishaji wa watoto kuondolewa.

DPP kupitia kwa kiongozi wa mashtaka Eugene Wangila alisema wanataka kesi hiyo iondolewe kwa kukosa mashahidi.

“Tunataka pia kesi hiyo iondolewe kwa sababu hatujapata mashahidi, ukosefu wa mashahidi utaathiri kesi hii,” alisema. Bw Wangila alisema upande wa mashtaka haijaweza kupata mashahidi wala kuandika taarifa zao ili kesi hiyo iweze kuendelea.

Kesi hiyo pia imekumbwa na tatizo na ukweli kwamba hakuna mfumo wa kisheria na wa kimaadili wa kusimamia mipangilio ya upasuaji nchini Kenya.

Ombi la kutaka kesi hiyo iondolewe ilifanywa siku chache baada ya Mahakimu Mwandamizi Mkuu Henry Nyakweba kutishia kutupilia mbali kesi hiyo ikiwa upande wa mashtaka hautaleta taarifa za mashahidi na stakabadhi muhimu katika kesi hiyo.

Hili ni baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha taarifa za mashahidi licha ya kufanya maombi kadhaa ya kutaka muda zaidi kuwasilisha mashahidi .

Bw Nyakweba alibainisha kuwa kushindwa kutoa taarifa za mashahidi imechangia kuchelewa kwa hiyo kesi kuendelea kinyume na sheria ambayo inapaswa kuwa ndani ya siku 21 baada ya kushtakiwa.

Wakati suala hilo lilipokuja mara ya mwisho, upande wa mashtaka uliomba muda ili kuwasilisha stakabadhi muhimu na mashahidi ,jambo ambalo lilifanya mahakama kuhairisha kesi hiyo , lakini mpaka sasa hawajafanya hivyo.

Katika kesi hiyo, Josephine Muthoni, Dkt Mahesh Chudasama na Neo Kian Fu wamekashtakiwa kufanya vitendo vinavyokusa biashara ya watoto.

Bi Muthoni na Dkt Chudasama wanadai kuwa tarehe tofauti kati ya Julai 16 na 28, kwa pamoja walimpa Kian mtoto mwenye umri wa siku 12 kwa uangalifu ili kuwezesha mtoto huyo kusafirishwa kutoka Kenya kwenda Singapore.

Bw Kian anahukumiwa kwa kuasili mtoto huyo kinyume cha sheria kwa lengo la kumsafirisha Singapore.