Habari Mseto

DPP ataka mganga aliyeachiliwa huru arejeshwe gerezani

March 10th, 2024 2 min read

NA BRIAN OCHARO

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma anaitaka Mahakama Kuu kumtupa gerezani mganga Stephen Vicker Mangira na wenzake watatu ambao waliachiliwa huru kwa kosa la utakatishaji fedha.

DPP amelalamika kuwa hakimu aliyewaacha huru watu hao miaka minne iliyopita alikosea kisheria kwa kufanya hivyo bila kuzingatia ushahidi uliowasilishwa.

“Hakimu alikosa kufahamu kwamba kulikuwa na ushahidi wa kutosha dhidi yao na hivyo kufikia uamuzi usio sahihi,” DPP alisema.

Upande wa mashtaka pia ulilalamika kuwa hakimu alishindwa kufahamu sheria kuhusu uzito wa ushahidi ulikuwa kwenye karatasi ya mashtaka.

Pia, serikali imedai kuwa mahakama ya hakimu ilikosea kuhitimisha kuwa kulikuwa na mkanganyiko katika maelezo ya walalamikiwa kukamatwa na mashahidi wa upande wa mashtaka.

“Hakimu alikosa kufahamu kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa watu hao walijuana na walikuwa pamoja siku hiyo. Walikubali ushahidi huu katika utetezi wao,” ODPP ilisema.

Upande wa mashtaka pia umeishutumu mahakama ya hakimu kwa kukosa kufahamu kuwa magari ya washtakiwa yote mawili yalikuwa sehemu moja wakati upekuzi ulifanyika na hata wakati magari hayo yalishikwa.

Mahakama ya Shanzu mnamo Mei 2021 ilimwachilia Bw Mangira na wengine watatu katika mashtaka kadhaa ikiwa ni pamoja na utakatishaji fedha, ulanguzi wa dawa za kulevya na kumiliki mali iliyoshukiwa kupatikana kinyume cha sheria.

Alishtakiwa pamoja na Nabil Loo Mohamed, Bakari Kila Bakari na Lilian Bernad Martin.

Bw Mangira alisema yeye ni mganga wa mitishamba aliyesajiliwa na alijipatia pesa kupitia kazi hiyo.Ili kurahisisha biashara yake, alisema anapata mitishamba yake kutoka kwenye misitu na milima au kama anavyoelekezwa na ‘malaika’.

Alisema kwenye karatasi zake za mahakama kwamba ana wateja nchini Kenya na kote ulimwenguni ambao wamethamini kazi yake kwa kumpa pesa taslimu au kumzawadia magari ya bei ghali kusimamia gharama ya matibabu.

Lakini kwa sababu serikali haikutoa ushahidi kupingana na utetezi wa Bw Mangira, mahakama ilimwachilia huru kutokana na mashtaka hayo.

Upande wa mashtaka, hata hivyo, umekata rufaa dhidi ya kuachiliwa kwao katika Mahakama Kuu.

Miaka miwili iliyopita, Bw Mangira alipoteza ombi la kurejeshewa magari ya bei ghali na zaidi ya Sh18 milioni pesa taslimu zilizochukuliwa kwake mwaka wa 2017.

Hii ilikuwa baada ya Mahakama Kuu mjini Mombasa kukataa kubatilisha uamuzi wa mahakama ya mahakimu iliyotupilia mbali ombi lake la kutaka arudishwe bidhaa hizo.Jaji Anne Ong’injo alibaini kuwa mahakama ya mahakimu haingetoa agizo la kuachilia vitu hivyo wakati kulikuwa na kesi mbili katikaMahakama Kuu na amri za kuhifadhi vitu hivyo.

Bw Mangira alikuwa amewasilisha ombi hilo katika Mahakama Kuu baada ya kuondolewa mashtaka ya jinai.