Habari Mseto

DPP ataka mnajisi aozee jela maisha sio miaka 20

October 16th, 2018 2 min read

Na BRIAN OCHARO

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji anataka kifungo cha miaka 20 dhidi ya mshukiwa wa unajisi kiwekwe kando, na kisha kufungwa maisha kwa kudanganya kuhusu umri wake.

DPP amewasilisha suala hilo mbele ya Mahakama Kuu ya Mombasa ili kuamua kuhusu hukumu hiyo ambayo ilitolewa wiki iliyopita na mahakama ya chini.

Ibrahim Hamisi Mohammed alishtakiwa kwa kosa la kunajisi msichana mwenye umri wa miaka saba na Ijumaa iliyopita, alihukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani baada ya kupatikana na hatia.

Upande wa mashtaka ulisema mshukiwa huyo alifanya kosa hilo mnamo Agosti 12, 2016 katika eneo la Mtongwe katika kaunti ndogo ya Likoni.

Mshtakiwa aliiambia mahakama kuwa alikuwa na umri wa miaka 18 wakati akitoa malilio , jambo ambalo upande wa mashtaka ulipinga ukisema haukuwa na thibitisho kuwa mshukiwa alikuwa na umri huo.

Upande wa mashtaka ulitegemea rekodi za polisi ambazo zilionyesha kwamba mtuhumiwa alikuwa na miaka 20 kwa fomu ya maelezo iliyojazwa katika kituo cha polisi.

DPP kupitia kwa Kiongozi wa Mashtaka , Bw Eugene Wangila alimkosoa Hakimu Mwandamizi Mkuu Henry Nyakweba kwa kutegemea ripoti ya awali ya hukumu ambayo haikuonyesha umri sahihi wa mtuhumiwa wakati akitoa hukumu.

Kiongozi wa Mashtaka Eugene Wangila alisema suala la umri wa mtuhumiwa halikutokea wakati wa majaribio na kwamba hakimu huyo aliendelea na kesi hiyo kwani alimchukilia mtuhumiwa kuwa mtu mzima tangu kesi hiyo ilipoanza.

“Hakimu huyo alitegemea ripoti ya kabla ya hukumu kuhusiana na suala la umri wa mtuhumiwa, na kwa kushangaza alikubali kwamba mshtakiwa alikuwa na miaka 18 wakati akihukumiwa,” Bw Wangila alisema.

Alisema kuwa ripoti hiyo ya kupotosha ya kabla ya hukumu ndio ilimfanya hakimu huyo kumfunga mshukiwa miaka 20.

Bw Wangila alisema upande wa mashtaka unataka Mahakama Kuu kubainisha kama ripoti ya awali ya hukumu ilikuwa na ushahidi wa kuaminika wa umri wa mshtakiwa ikilinganishwa na fomu ya maelezo ya polisi.

Bw Wangila pia alisema wanataka uamuzi ikiwa ilikuwa sawa kwa hakimu kutumia ripoti ya kabla ya hukumu kutozingatia Sheria ya Dhuluma za Kingono.

“Ni kwa sababu hizo ndio tunapendekeza kwa mahakama kuitisha rekodi za kesi hiyo kutoka kwa mahakama ya hakimu na kutoa maagizo sahihi kulingana na hukumu iliyowekwa,” alisema.

Kiongozi wa mashtaka alisema kuwa kulingana na sheria, mtu ambaye amenajisi mtoto mdogo anafaa kufungwa jela maisha.

Bw Wangila pia anataka mahakama kurekebisha suala hili na kufutilia mbali hukumu hiyo na kutoa amri inayofaa.

“Mahakama ya hakimu ilitoa adhabu isiyo halali na hukumu ambayo imesababisha mlalamishi na upande wa mashtaka kukosa haki , tunaomba mahakama hii kuangalia tena suala hili na kutoa uamuzi sahihi,” alisema.