Habari Mseto

DPP azimwa kumwondolea Ojaamong mashtaka

January 10th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumatano ilizima hatua ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kusitisha kesi dhidi ya Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong.

Jaji John Onyiego (pichani) aliamuru DPP akome kumwandama Ojaamong kisha aendelee na kuwasilisha ushahidi uliosalia.

DPP aliwasilisha ombi hilo katika mahakama kuu akiomba hakimu mkuu Douglas Ogoti anayesikiza kesi dhidi ya Ojaamong asimamishe kesi hiyo ndipo uchunguzi fulani ukamilishe kisha ushahidi uwasilishwe kortini.

Mawakili Danstan Omari na James Orengo walipinga hatua hiyo wakisema kuwa kesi dhidi ya Ojamong imesalia mashahidi wawili tu ikamilike.

“DPP ameona kuwa ushahidi aliowasilisha ni hafifu na anataka kuwasilisha mwingine mpya,” Orengo alimweleza Jaji Onyiega.

Mahakama ikitoa uamuzi ilisema DPP hakubaliwi kisheria kuwasilisha ushahidi mwingine.

“Ikiwa ushahidi aliowasilisha ni hafifu , basi hana budi ila kutazama kesi aliyomshtaki Ojaamong ikizama maji,” alisema Jaji Onyiego.

Mahakama ilisema haiwezi kutekeleza jukumu la kuwa msimamizi wa mahakama inayoamua kesi ya Ojaamong na kuagiza kesi iendelee.

DPP alikuwa amekata rufaa kupinga uamuzi wa Bw Ogoti kutupilia mbali ombi la kiongozi wa mashtaka DPP akubaliwe kuwasilisha ushahidi mpya.