Habari

DPP Haji atoa orodha ya washukiwa wa ufisadi kutoka makabila ya nchini Kenya

March 14th, 2019 1 min read

Na BENSON MATHEKA

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Noordin Haji, amezima wanaodai kuwa vita dhidi ya ufisadi vinalenga jamii moja kwa kuorodhesha idadi ya watu kutoka makabila tofauti walioshtakiwa kwa uovu huo.

Akiongea Jumatano usiku katika runinga ya Citizen, Bw Haji alisema kuna washukiwa 415 mahakamani kutoka makabila tofauti.

Kwenye orodha hiyo, washukiwa wengi wanaokabiliwa na kesi za ufisadi wanatoka jamii yua Wakikuyu ya Rais Uhuru Kenyatta.

Orodha yake inaonyesha kuwa watu 141 kutoka jamii hiyo wameshtakiwa tangu Bw Haji alipoingia mamlakani Aprili 2018.

Idadi ya washukiwa wa ufisadi kutoka jamii ya Waluo ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ni 56 ilhali 46 wanatoka jamii ya Wakalenjin ya Naibu Rais William Ruto.

Bw Ruto na washirika wake wa kisiasa wamekuwa wakilalamika kuwa watu kutoka jamii yao wanaoshikilia nyadhifa serikalini wanalengwa katika vita dhidi ya ufisadi.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Noordin Haji. Picha/ Maktaba

Siasa

Wamekuwa wakidai kwamba vita dhidi ya ufisadi vimeingizwa siasa.

Hata hivyo, Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa wakiwahimiza DPP na mwenzake wa upelelezi George Kinoti kuwakamata wote wanaopora mali ya umma bila kujali jamii au vyama vya kisiasa wanavyotoka.

Kwenye orodha ya Bw Haji, jamii ya Kisii ina watu 37 wanaokabiliwa na kesi za ufisadi, Mijikenda na Waswahili (34), Wakamba (31) na Waluhya (29).

Washukiwa wa ufisadi walioshtakiwa kutoka jamii za Wasomali ni 16, Wahindi ni 15 na Waembu ni watano. Kuna Waturkana watatu na Wamaasai wawili na Msamburu mmoja.

“Wewe ni mhalifu bila kujali kabila lako, unachofanya ni kuiba mali ya Wakenya na ni lazima ukabiliwe na mkono wa sheria. Inasikitisha tunajaribu kuingiza siasa katika suala hili,” alisema Bw Haji.

Bw Haji alitetea hatua ya kukamata washukiwa siku za Ijumaa akisema   ni mtindo ambao umekuwa ukiendelea tangu zamani.

Alisema mali yote iliyopatikana kwa njia ya wizi itatwaliwa.

“Hatutakushtaki na usukumwe jela kisha utoke baada ya miaka kumi  kufurahia mali ya uhalifu. Tunachofanya ni kufuata na kutwaa pesa hizo,” alisema.