Habari Mseto

DPP na EACC waonywa vikali na mahakama

August 13th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HAKIMU mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi mahakama ya Milimani alitoa agizo kali kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na Tume ya Kupambana na ufisadi nchini EACC dhidi ya kuwafikisha washukiwa kortini saa za alasiri.

“Kumekuwa na tabia isiyofaa kamwe. DPP na EACC huwazuilia washukiwa kwenye seli hadi saa za alasiri ndipo wanawafikisha kortini,” alilalamika Bw Ogoti.

Hakimu alisema kuanzia Alhamisi hakuna mashtaka yoyote yatakayokubaliwa na mahakama baada ya saa nane unusu kila siku.

“Ikiwa mashtaka yatafikishwa kortini baada ya nane unusu kila siku basi hayatapokewa,” aliamuru Bw Ogoti.

Hakimu aliamuru idara zote zinazohusika na uchunguzi zichukulie agizo hilo kwa makini..

Bw Ogoti alisema hayo baada ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero kufikishwa kortini saa tisa mchana na alikuwa ametiwa nguvuni Jumatano saa tano.