Michezo

DR Congo wapiga Guinea kuendelea kucheza ‘Lingala’ katika Afcon

February 3rd, 2024 1 min read

NA MASHIRIKA

‘CHUI’ wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walituma onyo kali kwa timu zilizosalia kwenye fainali za Kombe la Afrika (Afcon) zinazoendelea nchini Cote d’Ivoire baada ya kutoka nyuma na kupepeta Guinea 3-1 kwenye robo-fainali iliyochezewa katika uga wa De La Paix mjini Bouake.

Mohamed Bayo aliwaweka Guinea kifua mbele kupitia penalti ya dakika ya 20 iliyosababishwa na Chancel Mbemba.

Hata hivyo, Mbemba alisawazisha mambo dakika saba baadaye kabla ya DR Congo kufunga magoli mengine kupitia penalti ya Yoane Wissa na ikabu ya Arthur Masuaku kisha kutinga nusu-fainali ya Februari 7 jijini Bouake.

Hadi walipobandua Guinea, DR Congo walikuwa wameambulia sare katika mechi zao zote nne zilizotangulia huku wakidengua Misri kwa penalti 8-7 kufuatia sare ya 1-1 katika hatua ya 16-bora.

Masogora hao wa kocha Sebastien Desabre walianza kampeni za Kundi F kwa sare ya 1-1 dhidi ya Zambia kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Morocco kisha kutoka sare tasa dhidi ya Tanzania. Matokeo hayo yaliwavunia alama tatu, nne nyuma ya Morocco waliong’olewa na Afrika Kusini katika raundi ya 16-bora kwa mabao 2-0.

Guinea kwa upande wao walifungua Kundi C kwa sare ya 1-1 dhidi ya Cameroon kabla ya kukung’uta Gambia 1-0 na kukubali kichapo cha 2-0 kutoka kwa Senegal. Walifuzu kwa hatua ya muondoano wakiwa miongoni mwa timu nne zilizoambulia nafasi za tatu makundini kwa matokeo ya kuridhisha.

Hii ni mara ya kwanza kwa DR Congo kufuzu kwa nusu-fainali ya AFCON tangu mwaka wa 2015 wenyeji Equatorial Guinea walipowafunga penalti 4-2 kufuatia sare tasa kwenye pambano la kutafuta mshindi nambari tatu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO