Michezo

Drinkwater aharibiwa sura akijaribu kumumunya kidosho wa wenyewe

September 10th, 2019 2 min read

NA MASHIRIKA

NYOTA wa Chelsea ambaye kwa sasa anawachezea Burnley kwa mkopo, Danny Drinkwater, 29, alipokezwa kichapo cha mbwa msikitini wiki jana kwa jaribio kumshawishi kimapenzi mchumba wa mwanasoka mwenzake.

Kiungo huyo wa zamani wa Leicester City alilewa chakari katika baa ya Chinawhite jijini Manchester kabla ya kuanza kumtambalia mchumba wa mwanasoka Kgosi Ntlhe wa kikosi cha Scunthorpe United, Uingereza.

Baada ya kukataliwa na demu aliyemsisitizia kwamba alikuwa na mpenziwe wakati huo, Drinkwater alizua kizaazaa na purukushani za kila sampuli ndani ya baa.

“Sijali kabisa. Huyu ni kipusa wangu ambaye lazima anionjeshe asali leo, awe na mpenzi mwingine au la,” akasema Drinkwater huku akipayuka, kuropokoka bila ya kujidhibiti na kujigamba kuhusu jinsi anavyolipwa mshahara mnono wa hadi Sh13 milioni kwa wiki. Hali hii iliyowachochea mabaunsa sita wa kilabu hicho kumfurusha Drinkwater nje na “kumfuza adabu” kwa kumpiga kitutu.

“Walimrukia na kumvaa mzima mzima. Walimkunja na kumkanyaga vibaya wakitaka kumvunja miguu. Walifahamu kwamba ni mwanasoka wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na walipania kumzika kabisa kitaaluma. Damu ilitapakaa kila mahali,” akasema mdokezi aliyeshuhudia kisa hicho wakati akihojiwa na gazeti la The Sun.

Drinkwater ambaye anajivunia kuvalia jezi za Uingereza mara tatu, bado hajachezea kikosi cha Burnley katika jumla ya mechi tano zilizopita dhidi ya Southampton, Arsenal, Wolves, Sunderland na Liverpool.

Kichapo kilichomsaza na uso uliovimba, jicho lililoumia, mikono na mabega yaliyochubuka, shavu lililokatika na majeraha mabaya ya miguu kinatarajiwa kumweka mkekani kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Mwishoni mwa Julai 2017, Drinkwater alijinasia penzi la mwigizaji mahiri, mwanamitindo stadi na mwanahabari shupavu mzawa wa jiji la Manhattan, Georgina Leigh Cantwell, 29.

Georgina ambaye pia anajulikana pakubwa kutumia urembo wake kuwatia kishawishi wanasoka wenye hela nyingi ndani na nje ya bara Ulaya aliingia katika uhusiano wa kimapenzi na Drinkwater miezi saba baada ya kutemana na aliyekuwa mwigizaji mwenzake katika Big Brother, Jackson Blyton aliyerudiana na ‘Ex’ wake licha ya kumposa Georgina.

Pindi alipokatiza uhusiano na Leicester Cna kutua Chelsea mwanzoni mwa msimu huu, Drinkwater alitumia mtandao wake wa Instagram kuanzisha mawasiliano na Georgina.