Michezo

Drogba kuwania urais wa soka Ivory Coast

August 4th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

MAELFU ya mashabiki wa soka nchini Ivory Coast walijitokeza jijini Abidjan kumtilia shime Didier Drogba alipokuwa akiwasilisha stakabadhi za uwaniaji kabla ya kuzindua rasmi kampeni zake za kugombea urais wa Shirikisho la Soka la Cote d’Ivoire (IFF).

Drogba ambaye ni mwanasoka matata wa zamani katika kikosi cha Chelsea nchini Uingereza, atashindana na wawaniaji wengine wanne katika uchaguzi mkuu ambao umepangiwa kufanyika Septemba 5, 2020.

Ni matumaini ya Drogba, 42, kwamba mafanikio yake katika ulingo wa soka wakati akivalia jezi za timu ya taifa ya Ivory Coast almaarufu ‘The Elephants’ yatachangia kuchaguliwa kwake kudhibiti mikoba ya IFF.

Takriban barabara na vichochoro vyote vya jiji la Abijan vilijaa mashabiki waliojitokeza kwa wingi kumtia machoni nguli wao wa soka huku wakiwa wamebeba mabango na kuvalia mashati-tao yenye michoro ya picha za Drogba.

Licha ya kujivunia ufuasi mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka nchini Ivory Coast, Drogba bado hajapata idhini ya mwisho ya kuwa debeni.

Anahitaji kuteuliwa angalau na vikosi vitatu kati ya 14 vya Ligi Kuu na vingine viwili vinavyoshiriki ligi za madaraja ya chini katika soka ya Ivory Coast.

Mshindi huyo mara mbili wa taji la Mwanasoka Bora wa Mwaka barani Afrika, anahitaji pia kupendekezwa na angalau kundi moja la washikadau muhimu wakiwemo makocha, madaktari, marefa na wanasoka wa sasa na wa zamani.

Kufikia sasa, Drogba tayari amekabiliwa na pigo katika maazimio yake baada ya Chama cha Wanasoka wa Ivory Coast (IVFA) kukataa kuidhinisha ugombezi wake.

“Soka ni mchezo wa kila mtu kwa kuwa huwaleta watu pamoja. Tunaona hilo sasa hivi ikizingatiwa wingi wa mashabiki ambao wameandamana nami kuwasilisha stakabadhi zangu katika makao makuu ya IFF,” akatanguliza Drogba.

“Si siri kwamba soka yetu inaendeshwa vibaya na inaelekea pabaya. Hatutakubali mchezo huu kuzama tukiona. Ndio maana tumejitokeza na kusalia mstari wa mbele kuongoza ufufuo wa soka ya Ivory Coast,” akaongeza.

“Iwapo lengo langu si zao la msukumo wa ndani ya nafsi unaonipa motisha ya kurejesha hisani kwa soka ya Ivory Coast, basi nisingekuwa nasimama mbele yenu. Iwapo azma yangu si kuchangia maendeleo ya soka ya taifa letu na kwamba Mungu hakuhusika katika uwaniaji huu, basi nisingejitosa ulingoni kugombea urais wa IFF,” akaeleza Drogba.

Drogba alivalia jezi za Ivory Coast katika mapambano mbalimbali kati ya 2002 na 2014 ambapo alinogesha fainali tano za Kombe la Afrika (AFCON) na tatu za Kombe la Dunia. Hadi kufikia sasa, ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji bora wa muda wote kambini mwa Elephants kwa magoli 65 kutokana na mechi 105. Aliangika rasmi daluga zake mnamo Agosti 8, 2014.

Drogba ndiye mchezaji wa tatu baada ya Didier Zokora (123) na Kolo Toure (120) kuwahi kuwajibishwa mara nyingi zaidi na kikosi cha Ivory Coast.

Miongoni mwa wanasoka wa zamani wa Ivory Coast ambao wamejitokeza peupe kumuunga Drogba mkono katika azma yake ya kuwa rais wa IFF ni kiungo wa zamani wa Barcelona na Manchester City, Yaya Toure.

“Huu ndio wakati wa mabadiliko makubwa kufanyika katika soka yetu inayohitaji kuendeshwa kwa mtindo wa kisasa,” akatanguliza Yaya ambaye amewahi pia kuchezea kikosi cha Qingdao Huanghai nchini China.

“Ninaposema kwamba namuunga Drogba, eleweni kwamba ni kwa mustakabali bora wa soka ya Ivory Coast. Pia ni fahari kubwa kuwa na mwanasoka wa hadhi yake akitumikia taifa hili katika kiwango tofauti. Awekeze humu barani Afrika na maarifa yake yafaidi maelfu ya chipukizi wetu,” akaongeza Yaya ambaye ni kakaye beki wa zamani wa Arsenal, Man-City na Liverpool, Kolo Toure, 39.

Kati ya watakaopimana ubabe na Drogba debeni ni Naibu Rais wa IFF, Idriss Diallo na Sory Diabate ambaye atapania kuhifadhi wadhifa wake katika uongozi wa shirikisho hilo. Chama cha Wanasoka wa Zamani wa Ivory Coast (UFIFP) kinampigia chapuo Diabate.