Michezo

Droo moto Ulaya Manchester United, Arsenal wakipangwa na miamba

March 16th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

NYON, Uswizi

MITIHANI mikali inasubiri Manchester United na Arsenal katika Klabu Bingwa Ulaya na Ligi ya Uropa baada ya kukutanishwa na Wahispania Barcelona na Waitaliano Napoli, mtawalia.

Katika droo ya mechi za robo-fainali za Klabu Bingwa iliofanywa Ijumaa na Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA), Manchester City ya Pep Guardiola itapimwa makali dhidi ya Tottenham ilioajiri Mkenya Victor Wanyama, miamba wa Italia Juventus wakabiliane na Waholanzi Ajax nao Liverpool waliopoteza dhidi ya Real Madrid mwaka 2018, walimane na ‘mswaki’ Porto.

Mechi za robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya zitaandaliwa kati ya Aprili 9 na Aprili 17.

Mshindi wa mechi kati ya Spurs na City atamenyana na mshindi kati ya Ajax na Juventus katika nusu-fainali, huku mshindi wa mechi kati ya Barcelona na United akikibaliana na mshindi kati ya Liverpool na Porto katika nusu-fainali nyingine.

Mechi za nusu-fainali zitasakatwa kati ya Aprili 30 na Mei 8.

United ya Ole Gunnar Solskjaer imeshinda Barca mara moja katika mechi nane zilizopita.

Itaanza kampeni yake ya kutafuta tiketi ya nusu-fainali uwanjani Old Trafford ili isicheze mechi ya mkondo wa pili nyumbani wakati mmoja na majirani City.

‘Mashetani wekundu’ United walishinda taji la tatu na mwisho barani Ulaya mwaka 2008, mwaka ambao pia ndio walichapa Barca 1-0 katika nusu-fainali.

Mabingwa mara tano Barca wataingia mchuano dhidi ya United wakiwa na motisha ya kuwashinda katika mechi mbili zilizopita kwa jumla ya mabao 5-1. City itaanza mechi dhidi ya Tottenham na rekodi nzuri baada ya kubwaga vijana wa Mauricio Pochettino katika mechi tatu zilizopita. Wawili hawa wanatafuta taji lao la kwanza la Klabu Bingwa.

Mabingwa mara tano Liverpool hawajapoteza dhidi ya Porto katika mechi sita zilizopita wakichapa washindi hawa wa mataji matatu mara tatu na kutoka sare mara tatu.

Katika mechi hizo, Liverpool ilimiminia Porto mabao 12 na kufungwa mawili pekee.

Wafalme mara nne Ajax hawana ushindi katika mechi tatu dhidi ya mabingwa wa mwaka 1985 na 1996 Juventus wanaojivunia kuwa na mkali Cristiano Ronaldo.

Mnyonge

Mechi zingine za robo-fainali ya Ligi ya Uropa zitashuhudia Wahispania Villarreal na Valencia wakimenyana, Benfica (Ureno) ikikabiliana na Eintracht (Ujerumani) nayo Chelsea ilimane na mnyonge Slavia Prague (Czech).

Arsenal ilisalia mashindanoni kwa kulipiza kisasi dhidi ya Wafaransa hao 3-0 uwanjani Emirates, Alhamisi.

Pierre-Emerick Aubameyang aliongoza ufufuo huo alipocheka na nyavu mara mbili na kumega pasi ambayo Ainsley Maitland-Niles alifunga.

Rennes, ambayo ilishinda mkondo wa kwanza 3-1, ililalamika kwamba Aubameyang alifunga bao la pili akiwa ameotea. Emery alishinda mataji matatu ya Uropa akiwa Sevilla. Anataka taji hili katika msimu wake wa kwanza uwanjani Emirates.

Nayo Chelsea iliingia robo-fainali ya Uropa kwa kuaibisha Dynamo Kiev (Ukraine) 5-0 kupitia mabao matatu ya Olivier Giroud nao Marcos Alonso na Callum Hudson-Odoi wakafunga moja kila mmoja. Iliingia robo-fainali kwa jumla ya mabao 8-0.