Droo ya Dala Sevens yatangazwa, KCB na Strathmore kufufua uadui makundini

Droo ya Dala Sevens yatangazwa, KCB na Strathmore kufufua uadui makundini

Na GEOFFREY ANENE

VIONGOZI wa ligi ya raga za kitaifa za wachezaji saba kila upande mwaka 2022 KCB wamekutanishwa tena na Strathmore Leos kwenye duru ya Dala Sevens itakayofanyika jijini Kisumu mnamo Julai 2-3.

Droo ya duru hiyo ilifanywa Juni 22. Mabingwa watetezi wa Dala Sevens KCB waliofungua msimu huu kwa kunyakua taji la Kabeberi Sevens, na washindi wa Christie Sevens Strathmore watamenyana katika Kundi C pamoja na Impala Saracens na Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Wafalme wa Driftwood Sevens Mwamba wametiwa katika Kundi A. Watapepetana na Nondescripts, Nakuru na wenyeji Kisumu.

Kundi B linaleta pamoja Menengai Oilers, ambao walikamilisha Driftwood Sevens katika nafasi ya pili wikendi iliyopita, washindi wa Ligi Kuu ya wachezaji 15 kila upande Kabras Sugar pamoja na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Daystar na Masinde Muliro (MMUST). Timu ya Mmust imepata mwaliko baada ya kukosa Driftwood Sevens.

Homeboyz, Kenya Harlequin, Zetech Oaks na Catholic Monks wanakamilisha orodha ya washiriki wa mashindano makuu ya Dala. Wako katika Kundi D. KCB na Strathmore walikutana katika fainali ya Kabeberi na pia Christie.

Wanabenki wa KCB walizima Strathmore 12-10 katika Kabeberi nao Strathmore wakalipiza kisasi 25-10 katika Christie. Wote wawili walikosa kufika fainali ya Driftwood. Mashindano ya daraja ya pili ya Dala yamevutia timu 24 ambazo zimegawanywa katika makundi sita ya timu nne nne.

  • Tags

You can share this post!

Ruto azidi kuhusishwa na kesi ya ICC

IEBC yaita wawaniaji Jumatano

T L