Michezo

Droo ya mechi za kufuzu Afcon 2021 kufanyika Julai 18

July 5th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA itafahamu wapinzani wake katika kusaka tiketi kuingia Kombe la Afrika (AFCON) 2021 hapo Julai 18, 2019, baada ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kutangaza itafanya droo siku hiyo jijini Cairo nchini Misri.

Harambee Stars, ambayo bado inauguza kubanduliwa nje kwenye AFCON 2019 inayoendelea nchini Misri baada ya kuchapwa na Senegal 3-0 na Algeria 2-0 na kulemea Tanzania (3-2) katika mechi za Kundi C, imetiwa katika Chungu cha Tatu.

Chungu hiki kinajumuisha timu zinazoorodheshwa kutoka 13-24 barani Afrika. Vijana wa kocha Sebastien Migne hawatarajiwi kukutana na Guinea, Afrika Kusini, Cape Verde, Uganda, Zambia, Benin, Gabon, Congo Brazzaville, Mauritania, Niger na Libya katika mechi za kufuzu kushiriki makala hayo ya 33 kwa sababu timu hizi pia zinapatikana katika chungu hiki.

Chungu cha Kwanza kinachojumuisha timu zinazoshikilia nafasi ya kwanza barani Afrika hadi nambari 12 kina Senegal, Tunisia, Nigeria, Morocco, DR Congo, Ghana, Cameroon (wenyeji), Misri, Burkina Faso, Mali, Ivory Coast na Algeria.

Madagascar, Zimbabwe, Jamhuri ya Afrika ya Kat (CAR), Namibia, Sierra Leone, Msumbiji, Guinea-Bissau, Angola, Malawi, Togo, Sudan na Tanzania ziko katika Chungu cha Tatu.

Chungu cha Nne kinajumuisha Burundi, Rwanda, Equatorial Guinea, eSwatini (awali Swaziland), Lesotho, Botswana, Comoros, Ethiopia na washindi wanne wa awamu ya kuingia mechi za makundi.

Chungu cha Tano (mwisho) kinahusisha Liberia, Mauritius, Gambia, Sudan Kusini, Chad, Sao Tome & Principe, Ushelisheli na Djibouti. Eritrea na Somalia hazikujiandikisha kuwania tiketi 23 zilizoko mezani. Cameroon imeshafuzu kushiriki AFCON 2021 kama mwenyeji, ingawa itashiriki mechi hizi kujipa shughuli.

Vyungu vitano

Viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka Dunia vilivyotolewa Juni 14 vilitumika katika kuamua nyungu tano za washiriki 52 walioingia mechi za kufuzu.

Chungu cha Tano kinajumuisha timu zinazopatikana chini kabisa katika viwango hivyo barani Afrika.

Timu hizi zitapitia mkondo mrefu kufika AFCON 2021. Zitacheza mechi mbili za muondoano dhidi ya timu kutoka chungu hicho ili kupata tiketi ya kuingia mechi za makundi.

Awamu ya mechi za makundi itahusisha timu 48. Zitaganywa katika makundi 12 ya timu nne nne.

Mshindi wa kila kundi pamoja na nambari mbili watakuwa AFCON 2021.

Timu moja pekee kutoka kundi litakalokuwa na Cameroon ndiyo itajikatia tiketi.

Tarehe za mechi hizi za kufuzu pia zitajulikana wakati wa droo hapo Julai 18.