Michezo

Droo ya MIC inafanyika Ijumaa usiku

March 8th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya wavulana ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 15 itafahamu kundi lake la soka ya Mediterranean International Cup (MIC) droo itakapofanywa Ijumaa, Machi 8 usiku.

Mnamo Januari 23, 2019 Kenya ilithibitisha kushiriki mashindano haya yatakayofanyika Aprili 16-21 mjini Costa Brava nchini Uhispania.

Mbali na Junior Stars ya Kenya, timu zingine zitakazoshiriki kipute hiki ni Real Madrid, Barcelona, Villarreal, Celta Vigo, Valencia, Espanyol, Atletico Madrid, Real Betis, Malaga, Girona, Sevilla, Athletic Bilbao (Uhispania), Ajax Amsterdam, PSV Eindhoven (Uholanzi), Manchester United, Manchester City, Tottenham Hotspur, Crystal Palace, Everton (Uingereza), Lyon, Marseille, Paris Saint-Germain (Ufaransa), AS Roma, Inter Milan, Parma (Italia), Bayern Munich (Ujerumani), Besiktas (Uturuki), Porto (Ureno), Shakhtar Donetsk (Ukraine) na mataifa ya Mexico na Brazil.

Timu ya Kenya imekuwa ikipata mafunzo jijini Nairobi kutoka kwa kocha wa timu ya Harambee Starlets, David Ouma na pia kujipma nguvu dhidi ya timu mbalimbali.

Wachezaji 15 katika kikosi cha Ouma walikuwa katika timu ya Kenya ya Under-13 iliyoshiriki soka ya Southampton Cup nchini Uingereza mwaka 2016.