Habari

Duale adai nzige wamevamia bunge

February 19th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale ameibua kiwewe bungeni Jumatano alasiri alipodai kuwa nzige wameonekana humo.

Mbunge huyo wa Garissa Mjini amemtaka Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi atoe amri kwa walinzi wa bunge wathibitishe uwepo wa wadudu hao katika majengo ya bunge lakini ombi lake halikukubaliwa.

“Naibu Spika Moses Cheboi amenionyesha picha ya nzige ambayo alidai alipiga afisini mwake. Vilevile, wadudu hao wameonekana katika eneo la maakuli. Mpe Cheboi nafasi awaelezee wabunge ikiwa kweli wadudu hao wamevamia afisi yake,” akasema Bw Duale.

Mbunge wa Kitui Kusini Rachael Nyamai ameunga kauli hiyo mkono akisema kuwa yeye pia ameonyeshwa picha za nzige na Bw Cheboi ambaye pia ndiye mbunge wa Kuresoi Kaskazini.

“Mheshimwa Spika ni kweli kwamba nzige wamevamia majengo ya bunge. Mimi pia nimeona picha kwenye simu yake aliyopiga afisini mwake,” Dkt Nyamai akasema.

Hata hivyo, Bw Muturi amewapuuzilia mbali madai ya wabunge hao akisema “hili silo suala la kujadiliwa wakati huu. Tulieni.”

Awali, mwendo wa saa tano za asubuhi wabunge kutoka kaunti za Tharaka Nithi, Meru na Embu waliwahutubia wanahabari wakiwa wamebeba nzige wa rangi ya manjano.

Wakiongozwa na Mbunge wa Tharaka George Gitonga Murugara, wabunge hao waliitaka serikali kuweka mikakati thabiti ya kuzima wadudu hao waharibifu.

“Wadudu hawa wameangamiza mimea ya chakula, miti ya kahawa, miraa na nyasi inayotumiwa kama lishe ya mifugo wetu. Hili ni janga ambalo serikali inatatakikana kuwezeka raslimali nyingi za kupambana nalo. Hii isipofanyika uchumi wa eneo letu utaathirika pakubwa,” akasema Bw Murugara.

Kutoka Kushoto: Mbunge wa Tharaka George Gitonga Murugara, John Muchiri (Manyatta) na Geoffrey Kingangi (Mbeere Kusini) wahutubia wanahabari katika majengo ya bunge Februari 19, 2020. Picha/ Jeff Angote