Habari

Duale ameruka Ruto?

August 10th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Aden Duale, amechukua msimamo tofauti na mwandani wake wa kisiasa Naibu Rais William Ruto kuhusu maswala mbalimbali ya uongozi ukiwemo mchakato wa mageuzi ya Katiba.

Ingawa Dkt Ruto anapinga vikali marekebisho yoyote ya Katiba, Bw Duale ameunga mkono kwa dhati pendekezo la kubuniwa kwa wadhifa wa waziri mkuu mwenye mamlaka makubwa.

Dkt Ruto amekuwa akipinga juhudi zozote za kufanyia marekebisho katiba ya sasa akisema ni njama ya kuwatafutia waliobwagwa uchaguzini nafasi za kazi.

Vilevile, anadai hatua kama hiyo itawaongezea Wakenya mzigo wa kugharimia mishahara ya wanasiasa hao.

Ni kwa mintaarafu hiyo washirika wote wa karibu wa Dkt Ruto walionekana kususia vikao vya Jopo la Maridhiano (BBI) lililobuniwa na Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga.

Hii ni baada ya handisheki mnamo Machi 9, 2018, na lilipewa jukumu la kuangazia masuala tata ambayo yamekuwa yakizua migawanyiko nchini.

Naibu Rais na wafuasi wake wanahisi BBI ina njama fiche ya kumzuia kutwaa mamlaka ya kuongoza nchi baada ya muhula wa Rais Kenyatta kukamilika. Jopo hilo lilikamilisha vikao vyake jana.

Lakini akizungumza katika eneobunge lake la Garissa Mjini, Bw Duale alisema mfumo wa utawala wa Bunge ndio suluhisho pekee kwa mizozo ya mara kwa mara baada ya uchaguzi mkuu ambayo huikumba nchi.

“Kwa kuwa huwa tunapigana kuhusu uchaguzi wa rais, hali ambayo huzua taharuki nchini, sisi kama jamii za wafugaji tunapendekeza kubuniwa kwa mfumo wa utawala wa Bunge, ambapo Waziri Mkuu ndiye atakayekuwa kiongozi wa serikali,” akasema Bw Duale.

“Chama cha kisiasa ama muungano unaopata nafasi nyingi katika Bunge la Kitaifa na Seneti unapaswa kumteua Waziri Mkuu,” akaongeza. Bw Duale alitetea miito ya kuandaliwa kwa kura ya maoni, akisema hatua hiyo itakuza umoja wa kitaifa.

“Ushauri wangu kwa jopo la BBI, chini ya uongozi wa Seneta Yusuf Haji (Garissa) ni kutopoteza muda zaidi. Linapaswa, kwenye mapendekezo yake kupitisha mfumo wa utawala wa Bunge,” akasema.

Kura ya maamuzi

Dkt Ruto vilevile amekuwa akipinga maandalizi ya kura ya maoni, akisema Wakenya hawako tayari kushiriki katika shughuli nyingine ya kisiasa, hasa baada ya uchaguzi wenye utata wa 2017.

Akihutubu Chatham House, jijini London, Uingereza, Dkt Ruto alipuuzilia mbali miito ya kuandaliwa kwa kura hiyo, akisema inalenga kubuni nafasi kwa “viongozi waliokataliwa na wapigakura.”

Badala yake, alipendekeza kubuniwa kwa afisi ya kiongozi rasmi wa upinzani Bungeni.“Nimesikia baadhi ya mapendekezo ambayo yametolewa kwamba Serikali Kuu inapaswa kupanuliwa ili kubuni nafasi za waziri mkuu na manaibu wake wawili. Huko ni kuwaongezea Wakenya mzigo zaidi,” akasema.

“Tunachohitaji ni upinzani rasmi unaotambulika kikatiba. Pili, ikiwa nafasi hizo zitabuniwa, bado zitatwaliwa na chama kitakachoshinda uchaguzi, hivyo hilo halitaondoa taharuki za kisiasa,” akaongeza.

Mapendekezo ya kubuni wadhifa wa Waziri Mkuu pia yamekuwa yakitolewa mbele ya jopo hilo.

Jopo hilo litatoa ripoti yake ambayo linasema itasheheni mapendekezo yaliyotolewa na Wakenya wengi.