Habari MsetoSiasa

Duale aonya Kadhi Mkuu kuhusu Eid-Ul-Adha

August 20th, 2018 1 min read

Na JUMA NAMLOLA

KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Aden Duale ametishia kuitaka Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) imjadili Kadhi Mkuu kwa lengo la kumfuta kazi kwa madai ya kupotosha Waislamu.

Kwenye ujumbe mkali katika ukurasa wake rasmi wa Facebook, Bw Duale aklisema miongoni mwa mambo yatakayochunguzwa na Tume ya Huduma za Mahakama ni utumizi mbaya wa afisi.

“Tutapeleka malalamishi kwa JSC kujadili mienendo ya Kadhi Mkuu kuhusiana na utumizi mbaya wa mamlaka aliyopewa na Katiba ya Kenya,” akaandika Bw Duale.

Msimamo wake unatokana na kauli ya Kadhi Mkuu Sheikh Ahmad Muhdhar kumkosoa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i wa kutangaza kuwa Jumanne itakuwa Sikukuu ya Kitaifa kusherehekea Eid-Ul-Adha.

“Nilimwandikia mapema kumwarifu kuwa Waislamu Kenya tutasherehekea Idd mnamo Jumatano. Lakini waziri alipuuza barua yangu na kutangaza Sikukuu itakuwa Jumanne,” akalalama Sheikh Muhdhar. Lakini kwenye mtandao huo wa Facebook, Bw Duale alisisitiza kuwa Kadhi Mkuu alimkosea adabu Dkt Matiang’i kwa kukosoa uamuzi aliochukua.

“Hajj itakuwa kwa siku tano kuanzia Agosti 19 hadi 24. Siku ya pili ya Hajj hujulikana kama ‘Siku ya Arafa’ na huja siku moja kabla ya Eid Ul Adha. Kwa hivyo kulingana na kalenda ya Kiislamu, siku ya Arafat ni Jumatatu na Jumanne ndiyo sikukuu,” akaandika.

Mbunge huyo wa Garissa mjini anasema kulingana na Katiba, majukumu ya Kadhi Mkuu yapo wazi na kamwe hayahusu kuwatangazia Waislamu ni lini watasherehekea Idd. “Kadhi Mkuu anafahamu wazi katiba inasema majukumu yake ni kutatua mizozo ya sheria zinazowahusu Waislamu – ndoa, talaka na mirathi,” akaandika.