HabariSiasa

Duale aponea

June 2nd, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE wa Garissa Mjini Aden Duale ameponea na kuhifadhi kiti chake cha Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa katika mchakato unaoendelea wa kuwaadhibu wabunge waasi wa Jubilee.

Hata hivyo, katika mkutano wa kundi la wabunge wa chama hicho ulioongozwa na Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi Jumanne, wabunge Benjamin Washiali na Cecily Mbarire walipokonywa nyadhifa zao za Kiranja wa Wengi na Naibu Kiranja wa Wengi, mtawalia.

Nafasi ya Bw Washiali ilimwendea Mbunge wa Navakholo Emmanuel Wangwe na ile ya Bi Mbarire ikapewe Mbunge wa Igembe Kaskazini Maoka Maore.

Kabla ya kuanza kuwa mkutano huo, ilisemekana kuwa Duale ambaye ameshikilia wadhifa huo kwa miaka saba angeondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Mbunge wa Kipipiri Amos Kimunya.

Hata hivyo, duru katika mkutano huo ziliambia Taifa Leo kwamba wengi wa jumla ya wabunge 206 waliohudhuria walipinga pendekezo hilo.

Wakati huo huo, mabadiliko katika uongozi na uanachama wa kamati za bunge hazikufanyika. Lakini kiranja mpya Bw Wangwe alipewa muda wa hadi Juni 9 kufanya mabadiliko mbalimbali “yatakayoimarisha utendakazi wa kamati za bunge.”

Miongoni mwa mabadiliko ambayo yalitarajiwa ni kung’olewa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Bajeti Kimani Ichungwa na nafasi hiyo ipewe Mbunge wa Kieni Kanini Kega.

Mkutano huo ulisemekana kuhudhuriwa na wabunge 230 waliochaguliwa kwa tiketi ya chama cha Jubilee na vyama vingine shirika. Naibu Rais William Ruto ambaye ni Naibu Kiongozi wa Jubilee pia alihudhuria.

Kwenye mahojiano na runinga ya NTV Jumapili, Rais Kenyatta aliapa kutofanya kazi na viongozi ambao lengo lao ni kurudisha nyuma ajenda yake ya maendeleo.

“Hatutasita kufanya mabadiliko katika chama chetu n ahata serikali ili kwa kuondoa watu wasiounga mkono ajenda yangu na nafasi yao kupewa wale ambayo wamejitolea kufanikisha Ajenda Nne Kuu za maendeleo ambazo serikali yangu iliwaahidi Wakenya,” Rais Kenyatta akasema.