Duale ataka bunge kupunguza bei ya mafuta

Duale ataka bunge kupunguza bei ya mafuta

Na KNA

MBUNGE wa Garissa Mjini Aden Duale amelitaka bunge kushughulikia kwa haraka Mswada wa Ushuru wa Mafuta 2021, unaolenga kupunguza ushuru unaotozwa bidhaa za mafuta.

Bw Duale ambaye, zamani alihudumu kama Kiongozi wa Wengi katika bunge la kitaifa, alisema mswada huo utasaidia katika kupunguzwa kwa gharama ya maisha.

“Mswada huo unagusa maslahi ya wananchi na hivyo unapaswa kupewa kipaumbele badala ya miswada inayosaidia tabaka la wanasiasa,” akasema.

Bw Duale akaongeza: “Inavunja moyo kwa kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Amos Kimunya na mwenzake wa upande wa wachache John Mbadi kuwasilisha ombi kwa Spika aitishe vikao maalum kujadili mswada unaohusu masuala yanayowasaidia wananchi. Inaudhi kwamba tumeitwa mara tatu kufanya vikao maalum kujadili mswada wa marekebisho ya sheria za vyama vya kisiasa ili kuwasaidia wanasiasa kubuni miungano.”

Alisema mswada wa ushuru wa mafuta uliodhaminiwa na kamati ya bunge kuhusu fedha chini ya uongozi wa Bi Gladys Wanga, haujapewa kipaumbele.

Bw Duale ambaye alikuwa akiongea mjini Garissa Jumamosi, alisema kuwa atamwandikia barua Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, ili aitishe kikao maalum cha bunge hilo ili wabunge wajadili na kupitisha mswada huo wa kupunguza bei ya mafuta.

  • Tags

You can share this post!

Ajabu ya mjane kupoteza mamilioni kwa kupenda jini

Treni ya mizigo hadi Uganda kuanza Machi

T L