Habari za Kitaifa

Duale: Jenerali Ogolla alitumwa Bomas na wakubwa wake

April 21st, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Ulinzi Aden Duale amemtetea marehemu Jenerali Francis Ogolla dhidi ya madai kuwa ni miongoni mwa waliojaribu kubatilisha ushindi wa Rais William Ruto mnamo Agosti 15, 2022.

Akiongea Jumapili katika ibada ya mazishi ya mkuu huyo wa majeshi, Ng’iya, Kaunti ya Siaya Bw Duale alisema marehemu alitumwa na wakubwa wake katika ukumbi wa Bomas kwa sababu za kiusalama wala sio kuvuruga matokeo ya uchaguzi wa urais kwa sababu za kisiasa.

“Ningetaka kuthibitisha yale Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga alisema Jumamosi kwamba Jenerali hangeenda Bomas of Kenya kumlazimisha aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa IEBC kugeuza matokeo ya uchaguzi wa urais. Ogolla alinionyesha ujumbe mfupi kwamba alitumwa na wakubwa kudumisha usalama na sio kuingilia shughuli ya kujumuisha kura za urais,” Bw Duale akasema.

Waziri huyo alieleza kuwa Jenerali Ogolla, ambaye wakati huo alikuwa Naibu Mkuu wa Majeshi, hakuwa mwanachama wa Baraza la Kitaifa la Ushauri kuhusu Usalama (NSAC) linalongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma.

“Kwa hivyo, Jenerali Ogolla alitumwa huko na wakubwa wake ambao ndio waliokuwa wanachama wa NSAC. Baadhi ya waliomtuma wako hapa leo (Jumapili) na ninasema waziwazi kwa sababu mimi ni Mwislamu,” Bw Duale akafichua.

Waziri huyo aliongeza kuwa Jenerali Ogolla aliwahi kumpigia simu baada ya Rais Ruto kuingia afisini rasmi na kumweleza jinsi ambavyo tuhuma kwamba alienda Bomas of Kenya kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais zilimvuruga akili hadi kupunguza uzani.

“Alinipigia simu na familia inaweza kukubaliana nami kwamba tulijadiliana kwa kirefu, kwamba alipunguza uzani kwa sababu suala hili lilikuwa likimsumbua zaidi,” akasema.

Wakati wa ibada ya ukumbusho wa Jenerali Ogolla katika uwanja wa michezo wa Ulinzi, Nairobi, Bw Odinga alimwondolea marehemu lawama kuhusu tuhuma kwamba alijaribu kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais Agosti 15, 2022, katika ukumbi wa Bomas.

Akaeleza: “Jenerali Ogolla hakufika katika Bomas of Kenya kumlazimisha Chebukati (aliyekuwa mwenyekiti wa IEBC) kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais. Ninamjua alikuwa mwanajeshi aliyezingatia kazi yake. Tunataka hili suala likamilishwe tunapoomba Mungu aipumzishe roho yake pema.”