Habari

Duale kupinga kortini matokeo ya data za sensa

November 6th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

VIONGOZI wa eneo la Kaskazini Mashariki mwa Kenya wamesisitiza wataishtaki serikali kwa kutoa matokeo ya data za sensa ambazo haziwakilishi idadi kamili ya watu katika eneo hilo.

Wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge ka kitaifa Aden Duale wanesema Jumatano kwamba takwimu za eneo hilo zilikarabatiwa kuonyesha kupungua kwa idadi ya watu katika maeneo hayo ili kuyanyima rasilimali za maendeleo chini ya utawala wa ugatuzi.

“Hatuwezi kukubaliana na matokeo haya yanayoonyesha kuwa idadi ya watu katika kaunti ya Mandera, na maeneo bunge mengine katika eneo la Kaskazini Mashariki, imepungua kutokana sensa wa mwaka wa 2009. Hii haiwezekani kwa sababu wanaume kutoka jamii yetu huoana hadi wanawake wanne,” akasema.

“Msidhani kwamba mnaweza kukarabati takwimu kwa kupunguza watu wetu na kuongeza yenu.. tutaenda kortini wiki ujao kupinga matokeo haya. Shughuli ya kuongeza idadi ya watu huendeshwa katika chumba cha kulala sio katika vyumba vya mikutano katika afisi za serikali,” Bw Duale akaongeza kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.

Viongozi wa Kaskazini Mashariki wakiongozwa na kiongozi wa wengi katika bunge ka kitaifa Aden Duale (wa tatu mbele kushoto) wahutubia wanahabari katika majengo ya bunge Novemba 6, 2019. Picha/ Charles Wasonga

Mbunge huyo wa Garissa Mjini alikuwa ameandama na magavana Ali Korane (Garissa), Mohamed Abdi Mahmud (Wajir) pamoja na wabunge 18 kutoka eneo hilo.

Kulingana na matokeo hayo ambayo yalitolewa rasmi ya Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) idadi ya wanaume katika maeneobunge sita ya eneo hilo ilikuwa juu kulika ile ya wanawake, kinyume na hali halisi.

Maeneobunge hayo, kulingana na viongozi hao, ni kama Balambala, Lagdera, Mandera Mashariki, Mandera Magharibi na Fafi.

“Iweje kwamba shirika la KNBS inatuambia kuwa katika eneo bunge la Balambala idadi ya wanawake ni 35,000 ilhali ile ya wanaume ni 70,000. Ikiwa kuna idadi kubwa ya wanaume jinsi hii wataona nani?” akauliza Bw Duale.

Wakiunga mkono hatua ya kuwasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo hayo, magavana Korane na Mahmud wamesema matokeo yalikarabatiwa kufanikisha ajenda “potovu ya watu fulani ya kulemaza maeneo yetu kimaendeleo.”

“Hatutakubali njama kama hii kwa sababu tunafahamu fika kwamba ugavi wa rasilimali huenda sambamba na idadi ya watu. Hii ndiyo maana takwimu za maeneo ya Kati mwa Kenya na Rift Valley zimewekwa juu kimakusudi ili maeneo hayo yafaidi kimaendeleo,” akasema Bw Korane.