Habari

Duale motoni tena

June 8th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumatatu aliahirisha mkutano wa baadhi ya wabunge wa Jubilee wanaopania kumg’oa Aden Duale kutoka wadhifa wake wa kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa.

Kiranja wa Wengi – mnadhimu – Emmanuel Wangwe amesema Katibu Mkuu Raphael Tuju sasa ndiye atatangaza tarehe mpya ya mkutano huo ambao amesema ufanyika “hivi karibuni”.

“Ni kweli kwamba tulikuwa tumeitisha mkutano wa wabunge Jubilee katika makao makuu ya chama leo (Jumatatu) alasiri. Lakini baada ya mashauriano na kiongozi wa chama, imeamuliwa kuwa Katibu Mkuu ndiye atatoa mwaliko wa mkutano mwingine hivi karibuni,” amesema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge.

Alikuwa ameandamana na naibu wake, Maoka Maore.

Bw Wangwe, ambaye ni Mbunge wa Navakholo, amethibitisha kuwa yeye ndiye aliitisha mkutano katika makao makuu ya Jubilee, Pangani, Nairobi, kujadili hoja ya Mbunge wa Kieni Kanini Kega inayolenga kumwondoa mamlakani Bw Duale.

“Afisi yangu imepokea hoja hiyo na sahihi 126 za wabunge wa Jubilee wanaoiunga mkono. Ni hoja halali na imetimiza taratibu zote za kumwondoa kiongozi wa wengi kwa mujibu wa sheria za bunge nambari 19, ndiposa tumeiwasilisha kwa kiongozi wa chama,” akaeleza.

Mbw Wangwe na Maore wamekiri kwamba wao ni miongoni mwa wabunge walioweka sahihi zao katika hoja hiyo lakini wakafafanua kuwa walifanya hivyo kama wabunge wala sio vyeo vyao bungeni.

“Jina langu liko katika orodha ya wabunge hao 126 wanaounga hoja ya mheshimiwa Kega lakini sawa na naibu wangu, nimefanya hivyo kama mwakilishi wa watu wa Navakholo bali sio kama kiranja wa wengi,” Bw Wangwe amesema.

Bw Maore, ambaye ni Mbunge wa Igembe Kaskazini, ameeleza kuwa wakati wa Mkutano wa Kundi la Wabunge wa Muungano wa Jubilee (PG) uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi hatima ya Bw Duale haikuamuliwa.

“Hii ndiyo maana tumepokea hoja hii ya Bw Kega ili kutoa nafasi kwa wabunge kuamua ikiwa bado wana imani naye au la,” ameongeza.

Walipotakiwa kueleza ni kwa nini hatima ya Bw Duale haikuamuliwa waziwazi katika mkutano huo uliohudhuriwa na wabunge 112, Bw Wangwe akasema: “Rais hakutaka lawama. Alitaka wabunge washughulikie suala hilo kivyao na waamue ikiwa bado wanamwamini Bw Duale.”

Viongozi hao wawili hata hivyo hawakufichua sababu za kumtimua Bw Duale wakisema “sababu hizo zimeorodheshwa katika hoja hiyo.”

Hata hivyo, wiki jana Duale alipuuzilia kundi la wabunge wanaopania kumwondoa afisini akisema mpango wao hauna mashiko kisheria.

“Nina habari kwamba Bw Kega na wenzake wanakusanya sahihi kuniondoa. Nawaambia kuwa hiyo ni kazi bure na ambayo haiwezi kwenda kinyume na uamuzi wa Mheshimiwa Rais na Kiongozi wa chama cha Jubilee,” akasema kwenye taarifa katika majengo ya bunge.

Bw Duale alisema chama cha Jubilee kilimwidhinisha aendelee kuhudumu kama Kiongozi wa Wengi bungeni akiongeza kuwa wapinzani wake walifeli kutoa malalamishi yao katika PG.

“Nimezoea hoja kama hizo kutoka kwa Kanini Kega. Alileta hoja mbili aina hii katika bunge la 11 lakini ikafeli. Namshauri ajifahamishe na taratibu za kuteua na kuondoa viongozi wa bunge kisheria na atagundua kuwa mkondo anaofuata sio halali,” akasema.