Habari Mseto

Duale, Sakaja wavutania matumizi ya bustani za Central na Uhuru

April 18th, 2024 1 min read

NA WINNIE ONYANDO

GAVANA wa Nairobi Johnson Sakaja na Waziri wa Ulinzi, Aden Duale sasa wanavutania matumizi ya bustani za Central na Uhuru Park.

Waziri Duale, Jumatano alisema kwamba bustani hizo mbili hazifai kutumika kuandaa mikutano ya kisiasa.

“Hatutawaruhusu wanasiasa kuandaa mikutano yao ya kisiasa katika bustani hizo. Mpeleke mikutano yenu ya kisiasa kwingine ila sio katika bustani hizo. Wanasiasa watalazimika kutafuta ukumbi mwingine,” Waziri Duale alisema Jumatano alipofika mbele ya kamati ya Seneti.

Naye Gavana Sakaja akikabidhiwa bustani hizo mbili Alhamisi, alisema kwamba ni serikali ya kaunti ya Nairobi ndiyo itakayoamua matumizi ya bustani hizo.

“Ikiwa serikali ya Kaunti itaamua kuwa bustani hizo zitatumika kuandaa mikutano ya maombi, basi itakuwa hivyo,” Sakaja alisema.

Kando na hayo, gavana Sakaja aliwataka wakazi wa Nairobi kuzilinda na kutunza bustani hizo kwani zilikarabatiwa kwa ajili yao.

“Ni furaha kwamba bustani hizi zimefunguliwa rasmi kwa umma. Hivyo, nawarai wakazi wa Nairobi kuzitunza,” akasema Gavana Sakaja.

Kwa jumla, Sh1.18 bilioni zilitumika kukarabati bustani hizo mbili.

Wakati wa kukabidhi bustani hizo mbili kwa serikali ya Kaunti ya Nairobi, Sakaja na Duale walitia saini mkataba wa maelewano (MoU) kuhusu usimamizi wake katika kipindi cha mpito.

Ukarabati wa bustani hizo mbili ulioanza 2021 unakaribia kumalizika.

“Ni asilimia 8 pekee ya kazi zimesalia ikiwa ni pamoja na kuunganisha kisima kilichochimbwa katika Hifadhi ya Kati hadi tanki la maji na ujenzi wa bomba kuu ambalo limecheleweshwa kutokana na kazi zinazoendelea za KeNHA kwenye Barabara Kuu ya Uhuru,” Waziri alisema.

“Ili kuhakikisha tunamsaidia gavana, tumekubaliana tutaiacha nyuma timu yetu ya ufundi ikiwa ni pamoja na wahandisi na wasanifu majengo, kutia MoU ya kufanya kazi kwa kipindi cha miezi 6 ili kukamilisha zoezi hilo,” akaongeza Waziri Duale.