Dondoo

Dume lamkana mke aliyemfumania akitomasa kimada

October 22nd, 2018 1 min read

Na SAMMY WAWERU

Kiangoma, Nyeri

Kioja kilitokea katika baa moja mtaani hapa pale jamaa alipomkana mkewe aliyemfumania akiwa na mpango wa kando.

Jombi huyo alishangaza watu kwa kumkana mke wake hadharani, akidai kuwa hakumjua na hakuwa amewahi kumuona.

Inasemekana wawili hawa walikuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka 15 na wamejaaliwa watoto wawili.

Kabla ya tukio mke wa jamaa alikuwa akifikishiwa uhondo kuhusu mumewe aliyekuwa akionekana na msichana mmoja mtaani Kiangoma.

Alipomuuliza alikanusha, akimtaka kuepuka udaku wa watu.

Alimwambia akiendelea kuwasikiliza wadaku atavunja ndoa yao ya miaka mingi.

Majuzi baada ya mama huyo kupashwa ujumbe na wadaku wake, alifululiza hadi baa alikoambiwa mumewe alikuwa akijivinjari na kimwana.

Alifumania jamaa akimpakata mwanadada huku akimpokeza mabusu.

“Leo utasema wapashaji wangu wanakuonea na wanataka ndoa yetu isambaratike?”mama alichemka.

“Kwa hivyo huyu ndiye hukufanya ukose kufika nyumbani mapema na mshahara wote kuishia kwake?” alitaka kujua.

Jombi alionekana kutobabaishwa na kelele za mkewe. “Wewe ni nani? Kwa nini unataka kuniharibia ndoa yangu?” polo akiijibu.

Jamaa akishikilia kuwa hakuwa akimjua mke wake. “Huyu ni mume wangu na baba ya watoto wangu,” mkewe alisisitiza akitaja majina yake.Inasemekana kimwana alitokwa na kijasho chembamba lakini kalameni alimrai atulie.

“Mabaunsa wa hii baa wako wapi watoe huyu msumbufu hapa, hata sijawahi kumuona, leo ndiyo mara ya kwanza,” polo alimkana mkewe kabisa.

Kwa sababu ya aibu mama huyo alilazimika kuondoka akiapa kumtia jamaa adabu akirejea nyumbani. Baada ya jombi na kipusa wake kuburudika vya kutosha, waliondoka kila mmoja akienda kwake.