Dondoo

Dume lasingizia ujauzito wa mke kusaka ndogondogo nje

March 5th, 2024 1 min read

NA JANET KAVUNGA

NYALI, MOMBASA

KALAMENI wa hapa alikiri kwamba alishindwa kuvumilia hanjam na kuchepuka mara kadhaa mkewe alipokuwa mjamzito.

Jamaa alikuwa kilingeni na wenzake wakijadili tabia ya wanaume kuchangamkia vipusa hata wasio warembo kama wake zao.

Baadhi walikashifu wanaokosa kuwapamba wake zao kwa mavazi na vipondozi huku wakichangamkia wanaojikwatua na kuvutia.

“Mimi nilionja nje wakati mke wangu alikuwa mjamzito. Nilishindwa kuvumilia na kwa vile sikutaka kumsumbua katika hali ile, nilichovya mara kadhaa asali kutoka kwa mzinga mmoja tu nikitumia kinga. Kusema kweli asali ya wizi ni tamu lakini sikukubali inipagawishe,” jamaa alisema lakini wenzake wakamwambia wizi ni wizi tu.