Michezo

Duncan Otieno ayoyomea Zambia

November 14th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO Duncan Otieno anatarajiwa kuingia katika sajili rasmi ya kikosi cha Lusaka Dynamos kinachoshiriki Ligi Kuu ya Zambia (ZSL).

Otieno amekuwa akishiriki mazoezi na kikosi cha AFC Leopards tangu abanduke kambini mwa Nkana FC ambao ni mabingwa watetezi wa kipute cha ZSL.

Nyota huyo ambaye tayari ametua Zambia, anarejea kunogesha tena kivumbi cha ZSL ambapo anatazamiwa kutambulishwa rasmi kwa mashabiki wa Luska Dynamos mnamo Novemba 14, 2020.

“Lusaka wamekuwa wakiwania huduma za Otieno kwa muda mrefu sasa. Wametoa ofa nzuri ambayo ilikuwa vigumu kwa sogora huyo kukataa. Otieno ni mwanasoka wa haiba kubwa ambaye hatatizika kutulia haraka kambini mwa waajiri wake wapya ikizingatiwa kwamba amewahi kuchezea Zambia,” akasema mdokezi wetu kutoka shirika la Shujaa Sports Management (SSM) ambalo ni mwakilishi wa Otieno.

“Amefurahia sana kurejea Zambia na anatazamia kufanyia Dynamos makuu pindi baada ya kutia saini mkataba utakaorasimisha uhamisho wake,” akaendelea mdokezi huyo wa SSM.

Lukaka Dynamos wanajivunia pia huduma za beki mahiri wa Harambee Stars, Musa Mohammed aliyejiunga nao hivi majuzi baada ya uhamisho wake hadi Difaa El Jadidi ya Morocco kugonga mwamba.