Habari Mseto

EACC: Bunge kuamua ikiwa Mbarak anafaa kuongoza tume

December 17th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE Jumanne watafanya kikao maalum kujadili ripoti ya kuhusu ufaafu wa Twalib Mbarak aliyeteuliwa kwa wadhifa wa afisa mkuu mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).

Kulingana na notisi kwenye gazeti rasmi la serikali toleo la Desemba 18 Spika wa Bunge la kitaifa Justin Muturi alisema kikao hicho kitaanza saa tatu na nusu na kuendelea hadi saa nane na nusu alasiri .

Wakati huu wabunge wako katika likizo ndefu ambapo wanatarajiwa kurejea kwa vikao rasmi vya kawaida mwishoni mwa Februari, 2019.

“Kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na kwa mujibu wa sheria za bunge nambari 29 (3) za bunge nawajulisha wabunge na umma kwa jumla kwamba kikao maalum cha bunge kitafanyika mnamo Desemba 18, 2018 kuanzia saa tatu na nusu asubuhi,” ilani ilisema.

Iliongeza, “Lengo la kuitishwa kwa kikao hicho ni kujadili ripoti ya kamati kuhusu haki na masuala ya sheria (JLAC) kuhusu kupigwa msasa kwa aliyeteuliwa kuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC).”

Bw Mbarak, ambaye ni Afisa wa Usalama na Masuala ya Maadili katika kampuni ya kuzalisha umme nchini KenGen, aliteuliwa na usimamizi wa EACC mwezi jana baada ya kuwabwaga watu wengine 13 waliohojiwa kwa wadhifa huo.

Alipigwa msasa na kamati ya JLAC Ijumaa wiki jana katika majengo ya bunge ambapo aliahidi kupambana na zimwi la ufisadi bila woga wala mapendeleo.

“Nina ngozi ya kifaru. Kwa hivyo, endapo kamati hii itaidhinisha uteuzi wangu nitatekeleza majukumu yangu bila kuogopa mtu au asasi yoyote. Sitakubali kushawishiwa na mtu yeyote kwani, kisheria, EACC inawajibika kwa wananchi kupitia bunge,” akasema Bw Mbarak ambaye aliwahi kuhudumu kama afisa wa kijasusi katika jeshi la Kenya kabla ya kustaafu mnamo 1999.

Ikiwa uteuzi wake utaidhinishwa na bunge kesho, Bw Mbarak atamrithi Bw Halakhe Waqo ambaye hatamu yake ya miaka sita kama afisa mkuu mtendaji wa EACC inakamilika Machi, 2019.