Habari MsetoSiasa

EACC lawamani kutompa Sonko ushahidi

February 18th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

TUME ya Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) Juma nne ilishutumiwa na mahakama kwa kutowapa Gavana Mike Sonko na washukiwa wengine ushahidi kama ilivyoagizwa mwezi uliopita.

Hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Douglas Ogoti alishutumu afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na EACC kwa kutowapa ushahidi Gavana Mike Sonko na washukiwa wengine.

“Hii mahakama imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha kesi za ufisadi na huku ni afisi za DPP na EACC zinazokawia kuwasilisha ushahidi,” alisema Bw Ogoti.

Hakimu huyo alisema atasimama kidete kuhakikisha sheria imefuatwa na afisi za DPP na EACC ndipo haki itekelezwe katika kesi za ufisadi.

Bw Ogoti alisema hayo alipoelezwa na kiongozi wa mashtaka Bi Nanjala kwamba “nakala za mashahidi hazijakabidhiwa washtakiwa kufuatia agizo la mahakama kuu kwamba baadhi ya mashahidi wawekwe chini ya uangalizi wa kitengo cha kulinda mashahidi maalum (WPA).”

Kiongozi wa Mashtaka Bi Nanjala. Picha/ Richard Munguti

Hakimu alielezwa kufuatia agizo hilo la Mahakama kuu afisi ya DPP itaondoa ushahidi wa mashahidi watakaowekwa chini ya uangalizi wa WPA katika orodha na kuwapa majina bandia kabla ya kesi kusikizwa.

Mahakama ilielezwa nakala za ushahidi zimepewa washtakiwa isipokuwa washukiwa wawili Wambua Ndaka na Patrick Mwangangi.

Akihojiwa na Bw Ogoti afisa anayechunguza kesi hiyo Bw Idris Garane alisema hakuelewa barabara agizo la Janauri 27 2020 kwamba awape Bw Sonko na washukiwa wengine nakala za ushahidi katika muda wa siku 14.

Mawakili Cecil Miller, George Kithi, Prof Tom Ojienda na Paul Nyamondi walimweleza hakimu kwamba “hakuna ushahidi uliotolewa na afisi ya DPP ikiwa nakala za mashahidi hazipo.”

Bw Miller anayemtetea Sonko alisema “alikabidhiwa masanduku mawili ya ushahidi aliosema umepangwa vibaya.”

Wakili Cecil Miller. Picha/ Richard Munguti

Mahakama iliamuru washukiwa hao wapewe nakala za mashahidi kufikia Feburuari 25 kabla ya kesi kutajwa Februari 26 afisi ya DPP ieleze ikiwa imewapa ushahidi washtakiwa wote.

Bw Sonko alishtakiwa upya katika upokeaji wa Sh14milioni pamoja Antony Otieno Ombok.

DPP amefutilia mbali mashtaka dhidi ya Duncan Muchemi Njunji, Robert Muriithi Muna na Zablon Onyango Ochomo.

Na wakati huo huo Bw Ogoti alikataa jaribio la kumshtaki Bw Sonko kwa kesi nyingine ya tatu akisema maagizo ya hapo awali yalikuwa akabidhiwe nakala za mashahidi kabla ya kusomewa mashtaka mapya.