EACC yaambia Waiguru ‘tuliza boli’

EACC yaambia Waiguru ‘tuliza boli’

Na KNA

Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), imepuuza madai ya Gavana Anne Waiguru wa Kirinyaga kwamba uchunguzi inaofanya kuhusu madai ya ufisadi katika kaunti yake umechochewa kisiasa.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Twalib Mbarak alisema Bi Waiguru “anakimbia ubawa wake” kwa kuwa uchunguzi dhidi yake haujakamilika na faili kuwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) atakayeamua iwapo anafaa kukamatwa na kushtakiwa au la.

Mnamo Alhamisi, Bi Waiguru alidai kwamba EACC inapanga kumkamata kwa kuhama chama cha Jubilee na kujiunga na United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais William Ruto.Washirika wa Dkt Ruto kutoka Mlima Kenya pia waliishambulia EACC na Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) kwa kumhangaisha Bi Waiguru kwa kuhamia UDA.

Hata hivyo, akizungumza na wanahabari akiwa Mombasa, Bw Mbarak alisema uchunguzi dhidi ya Bi Waiguru ulikuwa ikiendelea hata kabla yake kujiunga na UDA na madai yake kwamba tume hiyo inanuia kumkamata yanalenga kutimiza maslahi ya kisiasa.

Bw Mbarak alisema uchunguzi wa madai ya ufisadi dhidi ya Gavana Waiguru ulianza akiwa katika chama cha Jubilee na kwamba hatua yake ya kuhamia UDA majuzi inaweza kuwa mbinu ya kutafuta huruma kutoka kwa umma ili kunusuru “maisha” yake ya kisiasa.

Kuligana na Bw Mbarak, faili ya uchunguzi dhidi ya Gavana Waiguru inapigwa msasa na wataalamu tofauti wa uchunguzi kabla ya kuwasilishwa kwa DPP aichunguze na kutoa mapendekezo yake.

“Mwanasiasa huyo anafuatilia kesi hiyo kisha anahamia chama kingine cha kisiasa, kisha anaanza kusema, ninahangaishwa. Faili ya gavana huyo hata haijafika kwa DPP. Iko ndani ya awamu za uchunguzi.

Ikiwa amepotoshwa na baadhi ya watu, ninamhurumia,” alisema Mbarak.Alihimiza wanasiasa wanaoamini kwamba EACC inatumiwa vibaya kusubiri uchunguzi ukamilike na faili kuwasilishwa kwa DPP.Mbarak alisema kwamba wanachunguza wanasiasa wa vyama tofauti vya kisiasa wakiwemo wa chama tawala na upande wa upinzani.

“Tumeshtaki magavana tisa kwa ufisadi. Baadhi ni wa ODM na Jubileea wanachoita Tangatanga na Kieleweke,” alisema.Alisema kwamba EACC ni tume inayozingatia sheria katika kazi yake na kwamba kabla ya kupendekeza mtu ashtakiwe, uchunguzi wa kina huwa umefanywa na ushahidi wa kuweza kuthibitisha mashtaka kupatikana.

“Tungo na mpangilio katika EACC. Hatuamki na kusema shtaki watu hawa. Chochote tunachofanya, mwishowe tunafika mbele ya korti huru na mshtakiwa huwa anaajiri mawakili wazuri na ikiwa kesi ni dhaifu, tunashindwa.

Kwa hivyo, sisi ni wazima kiasi cha kuwekelea mwanasiasa mashtaka ya uongo?,” alihoji.Mbarak alisema kwamba baadhi ya wanasiasa waliopora pesa za umma ameingiwa baridi kwa sababu EACC inafanya uchunguzi wa kina unaoshirikisha wataalamu na kwamba kuingizwa siasa katika vita dhidi ya ufisadi hakutazuia tume yake kutekeleza majukumu yake

You can share this post!

Kesi dhidi ya Ruto kuhusu unyakuzi wa nyumba kuendelea

Polisi waonya wanafunzi wanaochoma shule kuwa watafungwa...

T L