EACC yaelezea hofu ya fedha za serikali kuporwa uchaguzi ukinukia

EACC yaelezea hofu ya fedha za serikali kuporwa uchaguzi ukinukia

Na WALTER MENYA

ASASI za kuchunguza ufisadi zimeelezea hofu kuhusu kutokea kwa visa vya wizi na ubadhirifu wa pesa za umma kupitia ununuzi wa bidhaa kinyume cha sheria wakati huu uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia.

Magavana 22 wanaohudumu muhula wao wa pili watakuwa wakiondoka afisini, huku katika ngazi ya kitaifa utawala mpya utaingia mamlakani kwani Rais Uhuru Kenyatta atakuwa akiondoka baada ya kukamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho.

Kando na hayo, maafisa kadha wa umma, wanaoshikilia nyadhifa kuu serikalini watakuwa wakijiuzulu kufikia Desemba mwaka huu kuwania nyadhifa za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao unaoratibiwa kufanyika Agosti 9, 2022.

Kwa sababu hii, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), imesema inafuatilia kwa makini matumizi ya fedha za umma serikalini katika mwaka huu wa kifedha na mwaka ujao wa 2022/2023.

Kwenye mahojiano na Taifa Jumapili, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo, Bw Twalib Mbarak, alisema wameanza kupokea ripoti kuhusu ubadhirifu wa pesa za umma na “tutachukua hatua hivi karibuni.”

“Katika miaka ya nyuma, tumegundua kuwa makosa mengi hufanyika katika miaka miwili ya mwisho kuelekea uchaguzi mkuu, kuhusiana na usimamizi wa fedha za umma. Tunajua kuwa wanasiasa wengi sasa wanasaka fedha za kufadhili kampeni zao. Katika ngazi ya kaunti, maafisa wengi wanajaribu kuiba kwa kukiuka sheria za ununuzi bidhaa za umma kwa lengo la kufadhili ndoto zao za kisiasa,” Bw Mbarak akaeleza.

Afisa huyo anasema kwamba uchanganuzi wao umeonyesha kuwa ndani ya miaka miwili kuelekea Uchaguzi Mkuu, huwa kuna shughuli nyingi za ununuzi bidhaa na huduma na matumizi ya fedha hupanda.

Kando na hayo, huwa kuna msukumo mkubwa wa ulipaji wa malimbikizi ya madeni ya miaka mitatu iliyopita “kwa sababu ni kwa njia hiyo ambapo watu hujifaidi.”

“Tunashirikiana na maafisa wanaoshikilia vyeo vya juu katika utumishi wa umma. Kwa mfano, utapata kuwa mwanasiasa au waziri anamsukuma afisa fulani kuvunja sheria za ununuzi. Kwa hivyo, tunawaonya maafisa kama hao kwamba wakikubali kutekeleza uvunjaji sheria katika ununuzi, basi tutawaandama huku wale waliowasaidia watakuwa huru wakifurahia matunda ya uovu huo. Kwa hivyo, ili wawe salama tunawaomba wawe makini wasishawishiwe kuvunja sheria,” akasema Bw Mbarak.

Miaka miwili kabla ya chaguzi mbili zilizopita (2013 na 2017) kulikuwa na visa vya kupotea kwa fedha za umma kupitia matumizi yasiyozingatia sheria.

Kulingana na Bw Mbarak sakata kama hizi hutokea kwa sababu maafisa fulani wa umma hutaka kutumia mianya ya ulegevu wa asasi za kufuatilia matumizi ya fedha za umma, kama vile bunge, kutokana na shughuli za kampeni za kuwania nyadhifa za kisiasa.

Afisa huyo mkuu mtendaji wa EACC pia alitetea hatua ya tume hiyo kutamatisha uchunguzi kuhusu sakata ya ukodishaji wa ndege ya kifahari iliyotumiwa na Naibu Rais William Ruto katika ziara rasmi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).

You can share this post!

Madiwani watiwa presha kupitisha BBI

Elfsborg ya Joseph Okumu yang’aria Helsingborg msimu...