Makala

EACC yawinda mapapa, hali hii ikichochea siasa za kelele Mlima Kenya

May 15th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

HUKU Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini (EACC) ikiimarisha vita dhidi ya viongozi wafisadi, baadhi ya viongozi kutoka Mlima Kenya wameingiwa na wasiwasi.

Afisa kutoka EACC ambaye hakutaka kutajwa kwa sababu ya kutaka kulinda kazi yake, aliambia Taifa Leo kwamba tangu aliyekuwa Gavana wa Murang’a Mwangi wa Iria na mkewe kushtakiwa, kuna waziri mmoja ambaye ameingiwa na wasiwasi, akitumia kila mbinu kujinusuru.

“Kuna waziri ambaye ameingiwa na wasiwasi mkuu kwamba huenda akafutwa kazi na hatimaye akashtakiwa,” akasema mdokezi huyo.

Waziri huyo anasemwa kwamba amezindua misururu ya kutoa matamshi na kauli za kujiangazia kama aliye na uwezo wa kuanzisha vuguvugu jipya la siasa za upinzani katika eneo la Mlima Kenya ili kuwaogofya kisiasa Rais Willian Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Bw Twalib Mbarak bila kuthibitisha ni kina nani ambao wako kwa mtandao wa kunaswa na mtego wa mafisadi alisema “tuko na baadhi ya samaki wakuu wanaochunguzwa”.

Bw Mbarak alisema kwamba Kenya ikifanikiwa kupambana na ufisadi bila kuingiza mapendeleo na ukabila, wananchi wataweza kuishi maisha bora na kwa wepesi.

“Hili ni taifa lililobarikiwa ajabu na Mungu. Tuko na rasilimali na watu walio na ubunifu na bidii. Lakini ufisadi umetupokonya fursa za kustawi. Kuna mataifa ambayo hayana baraka ya rasilimali asili lakini yametupiku kimaendeleo. Sisi hapa kazi ni kujihusisha na ufisadi tu,” akasema Bw Mbarak.

Bw Mbarak alilalama kuwa ufisadi huo umejipenyeza katika vitengo muhimu vya huduma kwa wananchi kiasi kwamba umegeuka na kuwa janga.

“Ninyi ngojeni tu. Kuna mambo yatafanyika kwa kuwa vita hivi havina wa kupendelewa. Atakayechunguzwa na kisha ushahidi kupatikana bila shaka atashtakiwa,” akasema.

Tayari Bw Wa Iria na mkewe ambaye ni Bi Jane Waigwe Kimani, aliyekuwa Kamishna wa Kaunti Bw Patrick Mukuria na wengine Saba kwa wizi unaokisiwa kuwa wa Sh351 milioni.

Tayari kukamatwa kwao na kisha kushtakiwa kumeongeza joto la kisiasa eneo hilo, wafuasi wao wakisema wanalengwa kwa msingi wa kuwa wa upinzani. Ifahamike Bw Wa Iria anaegemea katika mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya unaongozwa na Bw Raila Odinga.

Inaaminika kwamba iwapo waziri huyo anayemulikwa atashtakiwa na afutwe kazi, basi ataingia mashinani kuzindua siasa za upinzani hivyo basi kuchafua siasa za eneo hilo.

Hapo awali, Bw Gachagua alikuwa amesema kwamba huwa na usemi mkuu kuhusu wa kupigwa kalamu na wa kutuzwa vyeo eneo la Mlima Kenya.