EACC yawazima Sonko na Baba Yao

EACC yawazima Sonko na Baba Yao

Na CHARLES WASONGA

GAVANA wa zamani wa Kiambu Ferdinand Waititu na mwenzake wa Nairobi Mike Mbuvi Sonko wamepata pigo baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuzima viongozi waliong’olewa mamlakani kuwania nyadhifa za umma.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumanne, Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Twalib Mbarak alisema asasi hiyo haitaidhinisha viongozi ambao wameondolewa afisini kwa kukiuka hitaji la Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili kuwania viti vyovyote katika chaguzi zijazo.

Lakini mnamo Jumatatu Msajili wa Vyama vya Kisiasa Anne Nderitu alimwidhinisha Bw Waititu, maarufu kwa jina, Baba Yao, kuwania wadhifa wa ugavana wa Nairobi kama mgombeaji huru.

Bi Nderitu alisema afisi yake imethibitisha kuwa Bw Waitutu sio mwanachama wa chama chochote cha kisiasa na alama yake haifanani na ya wagombeaji wengine.

Bw Waititu alitimuliwa afisini Januari mwaka huu kwa makosa ukiukaji wa Katiba, matumizi mabaya ya mamlaka na mienendo mibaya. Hii ni baada ya Bunge la Seneti kuidhinisha hoja iliyopitishwa na madiwani 63 wa Kaunti ya Kiambu.

Wakati huu Bw Waititu anakabiliwa na kesi ya kushawishi kupeanwa kwa zabuni ya kima cha Sh580 milioni kinyume cha sheria, Kesi hiyo ingali mahakamani na haijaamuliwa.

Lakini Jumanne jioni, EACC ilisema mtu ambaye ametimuliwa afisni kwa misingi ya ukiukaji wa hitaji la Sura ya 6 ya Katiba.

EACC inachukulia kuwa mtu kama huyo hajahitimu kuwania ikiwa;

  •  Ameondolewa afisini kwa kukiuka Sura ya Katiba au sheria wezeshi, kulingana na kipengele cha 75 (3) cha Katiba.
  •  Ikiwa alipatikana, kulingana na sheria, kwamba alitumia vibaya afisi ya serikali kwa njia yoyote inayokiuka sura ya sita ya Katiba inavyoelezwa chini ya vipengele vya 99 (2) (h) na 193 (2) (g).

Mtu kama huyo pia atazuiwa kuwania afisi ya umma ikiwa mahakama au asasi yoyote yenye uwezo wa kufasiri Katiba itampata na hatia ya kukiuka sura ya sita ya Katiba,” akasema Bw Mbarak katika taarifa hiyo.

EACC iliongeza kuwa ina idhini ya kuishauri IEBC kuhusiana na masuala ya maadili na hivyo haitaruhusu viongozi waliokiuka Sura ya sita ya Katiba kuendelea kushikilia afisi za umma.

Mbarak alisema EACC itawakagua wawaniaji wote watakaoshiriki katika chaguzi ndogo zijazo kuhakikisha na kuwasilisha ripoti yake kwa IEBC ili ichukue hatua zifaazo.

Afisa huyo pia alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha kuwa wanawachagua viongozi wenye maadili wakati wa chaguzi ndogo zijazo na hata katika chaguzi zingine kuu zitakazofanyika nchini miaka ijayo.

You can share this post!

2020: Wizi serikalini, migomo na ukosefu wa ajira corona...

Mwaka 2020 ulivyosambaratisha mipango ya Waititu