Habari MsetoSiasa

EACC yazimwa kupekuapekua maisha ya Kidero

November 1st, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA  kuu Alhamisi iliamuru tume ya kupambana na ufisadi nchini isipekuepekue makazi ya aliyekuwa Gavana wa Nairobi Bw Evans Kidero  kusaka ushahidi watakaotegemea kumfungulia mashtaka mapya.

Jaji Hedwig Ong’udi alikubalia ombi la Dkt Kidero baada ya kuelezwa na wakili Prof Tom Ojienda kuwa maafisa wa tume ya kupambana na ufisadi nchini EACC wamekuwa wakimsumbua gavana huyo wa kwanza katika jiji hili kuu nchini Kenya.

Jaji Ong’udi alisema kuwa ni jambo la kufisha moyo ikiwa maafisa wa EACC wameenda kwa Dkt Kidero kusaka makazi yake na afisi zake bila ya kupata kibali kutoka mahakamani.

Jaji huyo alifahamishwa kuwa shirika la kusaka mali iliyonunuliwa na pesa zilizoibwa kutoka kwa umma (ARA) limesisitiza Dkt Kidero hajaeleza jinsi alipata mali yake inayokisiwa kuwa  na thamani ya Sh9 bilioni.

Lakini Dkt Kidero amejitetea akisema alianza kufanya kazi akiwa na umri mdogo na alikuwa anapokea mishahara minonono.

“Nimekuwa nikilipwa mshara kwa Dola za Marekani na Pauni za Uingereza. Nilijilimbikizia mali nyakati hizo,” alisema Dkt Kidero katika ushahidi wake  kwqa mahakama.

Mahakama itatoa uamuzi Jumanne ikiwa maafisa wa EACC na ARA watazimwa kabisa  kupekuapekua afisi na makazi ya Dkt Kidero.

Pia mahakama itaamuru maafisa hao wakome kupekuapekua na kuchakura akaunti za mkewe Gavana huyu wa kwanza Nairobi , Dkt Susan Mboya.

“Kabla sijamuoa  Dkt Mboya alikuwa amejipatia mali. Kusumbuliwa anakosumbuliwa na Polisi hakufai kamwe. Haki zake zinakandamizwa. Lazima tabia hii ikome,” walisema Prof Ojienda na wakili James Ochieng Oduol.