Michezo

Eastern kumpata bingwa wa Chapa Dimba wikendi hii

February 7th, 2020 2 min read

JEFF KINYANJUI na JOHN ASHIHUNDU

MICHUANO ya mzunguko ya kuwania ubingwa wa Chapa Dimba na Safaricom nchini, wikendi hii itafanyika Kenyatta Stadium, Machakos kuwania ubingwa wa Kanda ya Mashariki.

Nusu-fainali zote zitachezwa kesho, Jumamosi, huku fainali ikifanyika Jumapili.

Mabingwa wa msimu uliopita – Supersolico kutoka Kaunti ya Mwingi na St Mary’s Ndovea kutoka Makueni zilibanduliwa katika hatua ya makundi, hivyo mabingwa wapya wataibukia kuwakilisha kanda hiyo ya Mashariki katika fainali za kitaifa zitakazofanyika mwezi Juni.

Katika nusu-fainali ya wavulana, Tumaini School kutoka Makueni itakutana na Biashara FC kutoka Moyale wakati Black Panthers ya Meru Central ikikabiliana na St Daniels ya Chuka.

Katika kitengo cha wasichana, Isiolo Queens itacheza na Mabuu Queens kutoka Moyale wakati Ngakaa Talent ya Makueni ikivaana na Chuka University.

“Kupitia kwa mashindano haya, vipaji mbali mbali vimetambuliwa kutoka mashinani na kupewa fursa ya kuzuru nchini Uhispania kujinolea katika viwanja maarufu vinavyotumiwa na timu kubwa za La Liga. Wakiwa Uhispania, baadhi yao wameweza kuvutia vituo vya kunoa vipaji pamoja na timu nyingine za hapa nchini,” alisema kocha Boniface Ndambuki wa Ngakaa Talent.

Washindi wa watapokea Sh200,000 huku watakaomaliza katika nafasi ya pili watapata Sh100,000.

Berlin FC kutoka Garissa inayopatikana eneo la Kaskazini Mashariki na Yanga FC ya Pwani kutoka Malindi pamoja na Kwale Ladies ni miongoni mwa timu zilizofuzu kwa fainali ya kitaifa, huku zikingojea kuwania zawadi ya Sh1 milioni.

Timu zingine zitakazoshiriki katika fainali hizo za kitaifa ni Falling Waters ya Laikipia kutoka Kanda ya Kati na Ulinzi Youth ya Nanyuki pia kutoka kanda hiyo.

Mafunzo ya kunoa vipaji kutoka kwa makocha waliopata vyeti vya La Liga tayari yamekamilika. Ya kwanza yalifanyika Mombasa mnamo Desemba huku mengine yakitarajiwa kufanyika Februari 22 na 23, Nairobi.

Baada ya fainali, wachezaji 32 watateuliwa kuunda kikosi kitakachozuru Uhispania kwa kambi ya siku ambayo itawapa fursa ya kupimana nguvu na timu za vijana nchini humo.

Ratiba ya nusu-fainali za Kanda ya Mashariki ni: Wavulana (Jumamosi):

Tumaini School na Biashara (saa nne unusu), Black Panthers na St Daniels (saa nane unusu).

Wasichana (Jumamosi): Isiolo Queens na Mabuu Queens (saa mbili unusu asubuhi), Ngakaa Talent na Chuka University (Saa sita unusu).