Habari

Eastleigh na Mji wa Kale hakuna kuingia wala kutoka kwa muda wa siku 15 zijazo

May 6th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

HAKUNA kuingia wala kutoka mtaa wa Eastleigh jijini Nairobi na Mji wa Kale ulioko Mombasa usiku na mchana kwa muda wa siku 15 zijazo kuanzia leo Jumatano.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema serikali imechukua hatua hiyo kutokana na ongezeko la visa vya maambukizi ya virusi vya corona katika mitaa hiyo.

Akitoa takwimu za maambukizi mapya ya Covid-19 ambapo watu 47 wamethibitishwa kuambukizwa corona kwa muda wa saa 24 zilizopita, Waziri amesema visa 32 vya maambukizi hayo vimeripotiwa mjini Mombasa, Mji wa Kale ukiwa na visa 18.

Aidha, Nairobi imekuwa na maambukizi mapya 11, mtaa wa Eastleigh ukitajwa kuwa na visa 5.

Busia imesajili visa 2 huku Kwale na Kiambu zikisajili kisa kimoja kila kaunti.

“Kutokana na ongezeko la maambukizi ya Covid-19 katika mtaa wa Easteligh, Nairobi na Mji wa Kale, Mombasa, hakuna kuingia wala kutoka kuanzia leo Mei 6, 2020, saa moja za jioni kwa muda wa siku 15,” waziri Kagwe ametangaza.

Serikali pia imeagiza masoko yote na mikahawa kufungwa mara moja.

Shughuli za uchukuzi mitaa hiyo miwili pia zimepigwa marufuku kwa muda wa siku 15.

“Hakuna kuingia wala kutoka Eastleigh na Mji wa Kale,” akasisitiza Kagwe.

Hata hivyo, Bw Kagwe amesema watu wanaruhusiwa kusafiri ndani kwa ndani katika mitaa hiyo, hasa kununua bidhaa kwenye maduka.

“Hatua hiyo itasaidia kulinda watu wa mitaa hiyo na maeneo mengine kuambukizwa corona,” akasema.

Idadi jumla ya walioambukizwa corona nchini imefika 582.

Takwimu za waliopona ni 190, lakini wawili wametangazwa kufariki kwa muda wa saa 24 zilizopita, idadi ya walioaga dunia kutokana na virusi vya corona ikifikisha 26.